Saturday, March 24, 2012

Wao wanavyodhania

MITUME wangewajua, ngazi wangeliachia,
Kwao haikutokea, wa chini kulala njaa,
Cha kwao walikitoa, kwenda watu kuwafaa,
Wao wanavyodhania, ukubwa ni kula sana!

Kidogo walitumia, bado wakawa na afya,
Huku wajimiminia, na maradhi yawajaa,
Kila ukiangalia, hekima inshapotea,
Wao wanavyodhania, ukubwa ni kula sana!

Mali wajilimbikia, nyuma zitazobakia,
Kaburi wakiingia, wengine kuzitumia,
Kwa dhambi na maasia, moto yanayochochea,
Wao wanavyodhania, ukubwa ni kula sana!

Busara wakitumia, kipato husimamia,
Mitaji ikachanua, na nchi kuinyanyua,
Watu juu wakishakuwa, ndipo nao kujifaa,
Wao wanavyodhania, ukubwa ni kula sana!

Njaa inawasumbua, kila kitu wakwapua,
Sahani kumi watwaa, wakati moja sawia,
Na kama kikibakia, ndani kinawaozea,
Wao wanavyodhania, ukubwa ni kula sana!

Wengi wanatarajia, wana kuja kuwafaa,
Wameacha mtegemea, riziki anayetoa,
Wao mungu wamekuwa, ya kwao wanayaamua,
Wao wanavyodhania, ukubwa ni kula sana!

Mchwa wameshazaliwa, kumega wanafuatia,
Ubahili walojaa, chao hakitabakia,
Ni lazima kitaliwa,na kitu kutosalia,
Wao wanavyodhania, ukubwa ni kula sana!

Na wanaokimbilia, wakubwa waende kuwa,
Kwa lengo la kujifaa, wao na zao jamaa,
Ukweli inatakiwa, wapate sasa kujua,
Wao wanavyodhania, ukubwa ni kula sana!

Ukweli inatakiwa, wapate sasa kujua,
Imechoka Tanzania, mirija kuingiziwa,
Viongozi wasozaa, ila kazi ni kuua,
Wao wanavyodhania, ukubwa ni kula sana!

Wanyonyaji kukataa, walaji wasiozaa,
Mali wanaochukua, kula na zao jamaa,
Au nje kuhamishia, hadi nchi kuishiwa,
Wao wanavyodhania, ukubwa ni kula sana!

Matonge wanaotia, mtoto asiyenyanyua,
Huruma wasojaliwa, ila kazi kubugia,
Njaa isowapungua, kila siku yazidia,
Wao wanavyodhania, ukubwa ni kula sana!

No comments: