Monday, March 26, 2012

Wangapi utawahonga?

HAMSINI milioni, hesabu Watanzania,
Mna ngapi milioni, wote kuwagawia,
Ukubwa mkauwini, na vinono kuopoa?
Wangapi utawahonga, milioni hamsini?

Hili naona utani, na litawageukia,
Wakaikosa thamani, nyani wanaotumiwa,
Moto uwe duniani, pamwe na akhera pia,
Wangapi utawahonga, milioni hamsini?

Hii kubwa nuksani, haki kwenda kununua,
Yamchukiza Manani, motoni huandikiwa,
Utapeta duniani, ila kesho utalia?
Wangapi utawahonga, milioni hamsini?

Nawaona majinuni, wanaifanya hadaa,
Kama vile ni utani, ya muda kuitikia,
Kumbe wako hatarini, milele watapotea,
Wangapi utawahonga, milioni hamsini?

Uwaonye Shukrani, bwana wa kuhurumia,
Hawa kama mumiani, si watu wa kujijua,
Wanatakiwa imani, kwao kuipalilia,
Wangapi utawahonga, milioni hamsini?

Wataishia motoni, macho wasipofumbua,
Ni ujinga wake nyani, hayawani alokuwa,
Kwanini na kisa gani, wakaja kuangamia?
Wangapi utawahonga, milioni hamsini?

No comments: