Tuesday, March 27, 2012

SI NCHI YA KUFANIKIWA!

Nje wanakimbilia, kwa hao wenye ulaji,
Huku wajititimua, wenda kusaka mitaji,
Kumbe wanang'ang'ania, kuujenga uhitaji,
Ndani isoangalia, si nchi ya kufanikiwa!

Uongo waliojaa, viongozi na walaji,
Kiburi wakajitia, wajione wajuaji,
Raia huwaumbua, mithili wakeketaji,
Ndani isoangalia, si nchi ya kufanikiwa!

Wanaokosa ulua, wakajaa ufujaji,
Fedha wakazitumia, ukata uwe wahiji,
Mola hatowaridhia, hata ikiwa Miraji,
Ndani isoangalia, si nchi ya kufanikiwa!

Wajuao kutumia, ila sio upataji,
Nchi huwa wanaua, nao ni wauaji,
Polepole inakuwa, lakini ni mauaji,
Ndani isoangalia, si nchi ya kufanikiwa!

Na chama kilichojaa, watu wababaihsaji,
Kazi kwake ni kulea, taifa la wahitaji,
Ombaomba walokuwa, kwa njaa na upataji,
Ndani isoangalia, si nchi ya kufanikiwa!

Viongozi wenye njaa, hufata wanunuaji,
Wakauza visokuwa, hata pia na mitaji,
Muda wote hulaaniwa, hawawi wafufuaji,
Ndani isoangalia, si nchi ya kufanikiwa!

Uongo ukienea, hakuna usahihishaji,
Kila pembe huingia, panya kwenye mifereji,
Mchana huko hukaa, na usiku watokaji,
Ndani isoangalia, si nchi ya kufanikiwa!

Hata paka wakitua, hushindwa ukamataji,
Maana hununuliwa, wakawa si wa kuchaji,
Kulamba wakaishia, wanaopewa ulaji,
Ndani isoangalia, si nchi ya kufanikiwa!

Kisa demokrasia, bado tunaihitaji,
Mbali iliyoenea, katika uchaguaji,
Uoza kuundoa, kwa kuwa wasafishaji,
Ndani isoangalia, si nchi ya kufanikiwa!

Nguvu kinapoachiwa, chama kimoja ulaji,
Wananchi wataumia, hakuna wa kuwafariji,
Nguvu sawia zikiwa, hapo kuna uponaji,
Ndani isoangalia, si nchi ya kufanikiwa!

Bunge linatakiwa, bila wachakachuaji,
Na idadi sawa kuwa, kwa wote wagombeaji,
Ikilazimu ikawa, mseto kwa uundaji,
Ndani isoangalia, si nchi ya kufanikiwa!

Ushindani maridhia, jambo la uiokoaji,
Mabaya hufichua, hakuna cha uzikaji,
Watu wawe kidedea, kuwafuta wajuaji,
Ndani isoangalia, si nchi ya kufanikiwa!

Watu wawe kidedea, kuwafuta wajuaji,
Kwa chama kisichotakiwa, kukataliwa ulaji,
Nje wakaondolewa, wabakie watakiwaji,
Watu wawe kidedea, kuwafuta wajuaji,
Ndani isoangalia, si nchi ya kufanikiwa!

Katiba inatakiwa, wananchi wawe majaji,
UUoza kuuondoa, kila wanapohitaji,
Na wala si kuzuiwa, na sheria za wafujaji,
Watu wawe kidedea, kuwafuta wajuaji,
Ndani isoangalia, si nchi ya kufanikiwa!

Raia wanatakiwa, wasiwe wasindikizaji,
Kila kitu kufuatia, na maamuzi kuhoji,
Kikiwa kisichokuwa, pawe na uwajibikaji,
Ndani isoangalia, si nchi ya kufanikiwa!

No comments: