Saturday, March 3, 2012

Kwa kila mwenye kujua

Alimu waliokuwa, vitabu wamepitia,
Wakajiona wajua, mengi tusiyoyajua,
Nadhari haijatulia, kama wasipotambua:
Kwa kila anayejua, yu juaye anayejua:

Zaidi anavyojua!



Kila unalolijua, hilo umezawadiwa,
Digrii moja huwa, kwenye kama tatu mia,
Na sitini kutimia, kama zilivyokadiriwa,
Kwa kila anayejua, yu juaye anayejua:
Zaidi anavyojua!

Na anayejitembua, hujua anachojua,
Ni kidogo kilokuwa, Adhari hajamfikia,
Na hatomfikia, hata elfu akipewa:
Kwa kila anayejua, yu juaye anayejua:
Zaidi anavyojua!

Yu juaye anayejua, kuliko anavyojua,
Kidogo ukigaiwa na vyema ukatumia,
Basi huongezewa, na visivyokadririwa:
Kwa kila anayejua, yu juaye anayejua:
Zaidi anavyojua!

Hujui unayejua, dunia hujaitambua,
Padogo unapoishia, ndiyo unayojaliwa,
Vingine haitakuwa, hili nalishuhudia:
Kwa kila anayejua, yu juaye anayejua:
Zaidi anavyojua!

Ni bure wajinyanyua, juu hautofikia,
Dari unshawekewa, kupita haitokuwa,
Na akili huishia, hapo ulipofikia:
Kwa kila anayejua, yu juaye anayejua:
Zaidi anavyojua!

Alaa wanisikia, hukumu utaitoa,
Ukweli kama najua, naomba nizidishia,
Yangu rahisi yakawa, siku hii yakaanzia:
Kwa kila anayejua, yu juaye anayejua:
Zaidi anavyojua!

Wapate kujionea, wanaonipuuziya,
Na bure kunichukia, kwa kweli kuwaambia,
Nawe utaamua, yao yatakayokuwa,
Kwa kila anayejua, yu juaye anayejua:
Zaidi anavyojua!

Tawhidi nalilia, na salama nitakuwa,
Chini yako kutembea, kadri itavyokuwa,
Pengine sintoingia, milango wakifungua,
Kwa kila anayejua, yu juaye anayejua:
Zaidi anavyojua!

Hapa hapa nabakia, najua utanifungulia,
Sina pa kukimbilia, ila hapa kupitia,
Naomba kunikadiria, ni mtumwa kwako nawa,
Kwa kila anayejua, yu juaye anayejua:
Zaidi anavyojua!

Machi 3, 2012.
Dar es Salaam. Tanzania.

No comments: