Monday, March 26, 2012

Mechi nimeiandaa

Wabunge tu kwa wabunge

Kiingereza kwa Kiingereza

Wabunge wanatakiwa, wajifanyo kujua,
Kiingereza kikawa, katikati chaelea,
Na sasa nimeamua, bungeni kwenda ingia,
Mechi nimeiandaa, kuzungumza ung'eng'e!

Kenya nimetembelea, na sababu kuzijua,
Na Uganda nako pia, majilisi nimetua,
Kiingereza wakijua, siwezi wakatalia,
Mechi nimeiandaa, kuzungumza ung'eng'e!

Tanzania tunajua, Kiswahili yatumia,
Tisini na tisa kwa mia, wote wankisikia,
Ila sasa mazoea, yameanza kuchipua,
Mechi nimeiandaa, kuzungumza ung'eng'e!

Wapo wanaojidhania, king'eng'e wanakijua,
Nami sitaki kataa, lao nawakubalia,
Spika nitamwingia, mechi apate niachia,
Mechi nimeiandaa, kuzungumza ung'eng'e!

Awamu kuichukua, king'eng'e tu kutumiwa,
Marufuku itakuwa, Kiswahili kukitia,
Hata neno moja kuwa, budi utaadhibiwa,
Mechi nimeiandaa, kuzungumza ung'eng'e!

Kusema watatakiwa, kwa ghibu kutumia,
Hakuna kuangalia, maandishi yalokuwa,
Fasaha mia kwa mia, lazima upate kuwa,
Mechi nimeiandaa, kuzungumza ung'eng'e!

Tivii nazitumia, rasmi yangu barua,
Zote zinakubaliwa, bungeni kwenda ingia,
Shindano kujionea, mambo yatakavyokua,
Mechi nimeiandaa, kuzungumza ung'eng'e!

Umbeya naukataa, eti komedi itakuwa,
Au Futuhi ikawa, mbavu watu kuumia,
Maana ninavyojua, Kiingereza mwakijua,
Mechi nimeiandaa, kuzungumza ung'eng'e!

Nahofu kuwasemea, wakubwa waheshimiwa,
Msininyime ridhaa, shindano kutofanikiwa,
Nami nawanyenyekea, hili mkalikubalia,
Mechi nimeiandaa, kuzungumza ung'eng'e!

No comments: