Saturday, March 10, 2012

Lenga roho

Lenga roho, ukitinga, mengine ninapangua,
Magoli nitayafunga, hata macho nisipokua,
Siihitaji mizinga, lugha ni bora silaha,
Lenga roho, ukilenga, moyo nitauchukua!

Si mlimbwende wa kanga, na malengo nayajua,
Kwetu hatuna kuringa, twajua kutumikia,
Utumwa unatuganga, wachawi watukimbia,
Lenga roho, ukilenga, moyo nitauchukua!

Si wa pete nazo shanga, viunoni twajivua,
Na wanaotusimanga, dunia huwaachia,
Ndoa hatuwezi funga, na kisichoendelea,
Lenga roho, ukilenga, moyo nitauchukua!

Ni watu wa kubananga, hatujui kubangua,
Kadiri ni kupuyanga, kipandio chatuumbua,
Tumejaliwa ujinga,na wajinga twajijua,
Lenga roho, ukilenga, moyo nitauchukua!

Thamani inatupinga, hatuwezi thaminiwa,
Na hata tukitabananga,kilo hatutazichukua,
Mizani yetu ukunga, kuzaa hatujkujaliwa,
Lenga roho, ukilenga, moyo nitauchukua!

Pwani wakishaboronga, iko siku twahamia,
Ukifutika uganga, ustawi utakuwa,
Ukiondoka ujinga, watu watajitambua,
Lenga roho, ukilenga, moyo nitauchukua!

Roho haiachi songa, kuendelea tabia,
Minyororo kuifunga, sio kinachotazamiwa,
Mtunzi siachi tunga, waovu kujafulia,
Lenga roho, ukilenga, moyo nitauchukua!

No comments: