Sunday, March 11, 2012

Wajinga ndio waliwa

Majuha wanatumiwa, na wajinga wanaliwa,
Ndivyo inavyotokea, vingine haitakuwa,
Na wachache wanajua, vipi watalizuia,
Wajinga ndio waliwa, na majuha watumiwa!

Elimu inapovia, na njaa ikazidia,
Akili hujafifia, na msukule ukawa,
Unga washindiliwa, utamu hutojujua,
Wajinga ndio waliwa, na majuha watumiwa!

Waishi walojaliwa, na mtaji kutuibia,
Kotekote kutanua, jinsi wanvyochagua,
Nini utawaambia, na nchi wameinunua?
Wajinga ndio waliwa, na majuha watumiwa!

Elimu watachafua, ujinga ukazagaa,
Wajinga wakishajaa, utawala wachukua,
Nani atakayejua, nchi wanavyojilia?
Wajinga ndio waliwa, na majuha watumiwa!

Starehe huridhiwa, kwenye makazi kujaa,
Njenje changudoa, mitaani wazagaa,
Na pombe soko huria, yoyote ukachagua,

Lengo wameshaamua, mlewe na kutojitambua,
Wao wapate zengea, kila kinachowafaa,
Na ulevi ukiwaachia, nchi wameshajiuzia,
Wajinga ndio waliwa, na majuha watumiwa!

Uongo watauzua, matope kunipakaa,
Ukweli nikiutoa, chinichini kuzimia,
Hali haki waijua, ndiyo inayoangamia,
Wajinga ndio waliwa, na majuha watumiwa!

Nchi itatawaliwa, na kitu wasiojua,
Na mipango kutumbua, iwe isyotufaa,
Arijojo kujendea, angani tukapotea,
Wajinga ndio waliwa, na majuha watumiwa!

Haya nimewaachia, ajenda kuziandaa,
Mapema mkaamua, ni yepi kuzungumzia,
Vingine hapatabakia, kiwezacho kuwafaa,
Wajinga ndio waliwa, na majuha watumiwa!

No comments: