Monday, March 26, 2012

Iko aiku mtaingia

Kidela kasimulia, simulizi kazishika,
Kichwa anaugulia, kawachokoza mzuka,
Sasa wanahadithia, ibura zinazozuka,
Iko aiku mtaingia, kutoka sintowaachia!

Ajua wanaojua, hata kwao keshafika,
Ni watu wa kutangulia, japo sio wa kufika,
Mwendo wao kutembea, kitako hakijakalika,
Iko aiku mtaingia, kutoka sintowaachia!

Msongo umeshapaa, mhemuko wa mzuka,
Juu mtu ahemea, ataka kupumzika,
Kivuli kakusudia, wanakataa mzuka,
Iko aiku mtaingia, kutoka sintowaachia!

Miye hubaki kucheka, ni wasioelekeka,
Mbuyu wauparamia, ujuha unaofanyika,
Hali walishatakiwa, mbuyu kuuzunguka,
Iko aiku mtaingia, kutoka sintowaachia!

Acha kuyafikiria, ya karibu kufanyika,
Macho ukifungua, mbali utatahadharika,
Kujenga asiyepewa, utamlaumu kubomoka?

Ngazi inayotitia, walaumu kuporomoka?
Na juu wanaokuwa, wajua chini watafika?
Kaa juu shikilia, mimi na yangu naondoka,
Iko aiku mtaingia, kutoka sintowaachia!

Upambe naukataa, fikra nitazitoa,
Mtu ukimtumia, wengine kudhulumika,
Hakika mwenye hatia, hubaki ni mhusika,
Iko aiku mtaingia, kutoka sintowaachia!

Kigingi kimebakia, kisiki hutoepuka,
Mbona ningeshachukua, ningehitaji miliki,
Kunyonya sikuzoea, wala sinayo ashiki,
Iko aiku mtaingia, kutoka sintowaachia!

Hapahapa nabakia, fikra kugawanyika,
Chema nikatumikia, na bora kujazalika,
Hadithi kusimulia, kizazi kisicho shaka,
Iko aiku mtaingia, kutoka sintowaachia!

No comments: