Saturday, March 31, 2012

Tumezoea majembe

Nawasema kuurumbembe, waliokubuhu vijembe,
Vichwa vyao wasivimbe, kuwasifu nisiambe,
Ninawaona ni ng'ombe, kuchinjwa wao ujumbe,
Tumezoea majembe, havitushindi vijembe!

Niacheni niwachambe, wanaokifu wajumbe,
Hata kitu wasirambe, kwenye hizo zao tembe,
Na popote wasitambe, bado ni wala maembe,
Tumezoea majembe, havitushindi vijembe!

Ajira yao waimbe, ili watu wasigombe,
Hutaka vichwa wavimbe, wavipate na vikombe,
Kwa kuzing'oa pembe, na kumwaga nyingi pombe,
Tumezoea majembe, havitushindi vijembe!

Wanataka uwalambe, na ya kwao uyaimbe,
Kama sivyo wakukumbe, wakuchanje kwa uwembe,
Macho yako wakufumbe, ya ovyo usiwachambe,
Tumezoea majembe, havitushindi vijembe!

Nendeni mkawabambe, huku wamevaa pembe,
Ni majini msiombe, mkutane na wazembe,
Bilauri na vikombe, huvitumia wachambe,
Tumezoea majembe, havitushindi vijembe!

Nalipika langu sembe, na mchuziwe wa shombe,
Vinginevyo usiambe, riziki yangu si chembe,
Pawa tila ni uvimbe, kwanini mguu usivimbe ?
Tumezoea majembe, havitushindi vijembe!

Nanywa hili langgu kombe, majirani msisambe,
Nitazikomesha ngebe, vya kwangu wasiviibe,
Niwafungie mikebe, wasikike wasitambe,
Tumezoea majembe, havitushindi vijembe!

Hatuogopi vijembe, tumezoea majembe,
Vinginevyo msitambe, wimbo wenu tuuimbe,
Na siku ya siku tugombe, mchawi wetu tumzombe,
Tumezoea majembe, havitushindi vijembe!

No comments: