Monday, March 26, 2012

Mwiba ng'ombe au yai

Taarifa zaingia, uwizi umefanyika,
Kituoni naingia, zamu yangu kuishika,
Faili nimeletewa, notisi imeandikwa,
Mwiba ng'ombe au yai, nani ni jambazi wa kweli ?

Mkubwa kashikwa wizi, ng'ombe wa mtu kateka,
Walofanya fumanizi, kwao sasa ni mateka,
Wanangoja maamuzi, polisi twende mdaka,
Mwiba ng'ombe au yai, nani ni jambazi wa kweli ?

Kisha eti kuna mwizi, yai moja kalipoka,
Tena kaiba majuzi, mwibiwa hana hakika,
Hana habari dokozi, kama alikwishapoka,
Mwiba ng'ombe au yai, nani ni jambazi wa kweli ?

Duni vifaa vya kazi, kituo chafilisika,
Natakiwa maamuzi, mara moja kufanyika,
Bodaboda ya makzi, ipate kwenda tumika,
Mwiba ng'ombe au yai, nani ni jambazi wa kweli ?

Nikaamua upuuzi, kesi ya yai yafutika,
Koplo kumpa kazi, mkubwa kwend a kumshika,
Mara simu fululizi, zasema siwezi mshika,
Mwiba ng'ombe au yai, nani ni jambazi wa kweli ?

Nikafanya ugunduzi, koplo kumbe atumika,
Mkubwa kampa kazi, nami kushughulika,
Amri kaweka wazi, bosiwe kaelimika,
Mwiba ng'ombe au yai, nani ni jambazi wa kweli ?

Kuuliza siliwezi, neno limegundulika,
Kumbe kuna wengine wezi, kamwe huwezi washika,
Hawa ni wa ndani wezi, daima wanalindika,
Mwiba ng'ombe au yai, nani ni jambazi wa kweli ?

No comments: