Thursday, March 8, 2012

Kiumbe usiwe nzi

Ninakuasa mpenzi, uliye wangu azizi,
Usije ukawa nzi, kwa watu haupendezi,
Na kwa mume ni maudhi, wala hutapata hadhi,
Kiumbe usiwe nzi, mumeo utamuudhi!

Nzi kiumbe ajizi, kuishi naye huwezi,
Uchafu anauenzi, na uoza kikwatuzi,
Harufu mbaya dowezi, ni wake utandawazi,
Kiumbe usiwe nzi, kwa watu haupendezi!

Kwa vidonda hajiwezi, na jeraha ni makazi,
Ndizo zake simulizi, nyinginezo haziwezi,
Kuvipenda ni mjuzi, aupenda ugunduzi,
Kiumbe usiwe nzi, mumeo utamuudhi!

Kwa wengi huwa maudhi, mkubwa king'ang'anizi,
Na kisha ni mchafuzi, na kinyaa mtengezi,
Ukifanza fumanizi, kumuua siyo kazi,
Kiumbe usiwe nzi, kwa watu haupendezi!

Nakuasa la azizi, usiwe kama ni nzi,
Ya kwako kuwa ushuzi, ya mkia na mkizi,
Karaha mimi siwezi, ninapenda utulizi,
Kiumbe usiwe nzi, mumeo utamuudhi!

Na maswali siyawezi, yatokayo kama uzi,
Na kichwa ni simaizi, sembuse yenye radhi?
Naona ni uchochezi, na uhaini siwezi,
Kiumbe usiwe nzi, kwa watu haupendezi!

Penzi ni kubwa hifadhi, wajuao humaizi,
Linataka utambuzi, mwenzio ukamuenzi,
Ukajua maamuzi, yafaayo kila mwenzi,
Kiumbe usiwe nzi, mumeo utamuudhi!

Penzi lataka mahadhi, na wimbo wenye utunzi,
Yakawa masimulizi, mwilini yatia ganzi,
Na raha yenye uzuzi, na akili uvumbuzi,
Kiumbe usiwe nzi, kwa watu haupendezi!

Lataka matengenezi, pia mkubwa ujenzi,
Na kisha usimamizi, udhibiti na majazi,
Ashakum kunradhi, kila palipo tatizi,
Kiumbe usiwe nzi, mumeo utamuudhi!

Mapenzi kama jahazi, nahodha wawe wajuzi,
Lataka usimamizi, na bora maelekezi,
Wote kuwa viongozi, kuupata ufunguzi,
Kiumbe usiwe nzi, kwa watu haupendezi!

Ukikosa kiyoyozi, kipepeo kukienzi,
Ikiwa hujitulizi, haya hauyawezi,
Utakuwa kama nzi, kwa mwenzi kuwa maudhi,
Kiumbe usiwe nzi, mumeo utamuudhi!

Pendo lataka utenzi, na wala sio hirizi,
Mwenzio ukamuenzi, kwa akili za saizi,
Abakie hajiwezi, kwa weledi na ujuzi,
Kiumbe usiwe nzi, kwa watu haupendezi!

Tabasamu ukienzi, hulainika azizi,
Mbali na wewe hachezi, sikuzote akuenzi,
Hutoona uvamizi, wala kamwe udowezi,
Kiumbe usiwe nzi, kwa watu haupendezi!

Usafi ukiuenzi, nyumba huwa ni azizi,
Hayatokufa mapenzi, kwa dawa wala mizizi,
Joho mtalidarizi, lal utukufu wa enzi,
Kiumbe usiwe nzi, kwa watu haupendezi!

Mkimpenda Mwenyezi, na yeye kwenu Azizi,
Atawapeni makazi, yenye neema na hadhi,
Akawapandisha ngazi, kiyama kitakapojizi,
Kiumbe usiwe nzi, kwa watu haupendezi!

No comments: