Saturday, March 10, 2012

Dini pasi kuongoza

Wazungu wanatuambia, sekula yaabudiwa,
Ukafiri ulokua, na nguvu ya kisheria,
Nami ninaukataa, muumini naamua,
Dini pasi kuongoza, yazuka maangamizi!

Wakubwa watatokea, Amerika na Ulaya,
Ushoga wakaamua, milango kufungulia,
Uchamungu ukipwaya, haya budi kutimia,
Dini pasi kuongoza, yazuka maangamizi!

Jambazi tutaachia, nchi wakaichukua,
Wakatumia sheria, vya wizi vikawafaa,
Wale wanaoibiwa, wao ndio wezi wakawa,
Dini pasi kuongoza, yazuka maangamizi!

Watairidhi zinaa, mikutanoni ikawa,
Vyama kushangilia, maisha wafurahia,
Shetani akaingia, na zaidi kuwazuzua,
Dini pasi kuongoza, yazuka maangamizi!

Tutaridhia malaya, ya kwetu kusimamia,
Mikosi ikaingia, kila wanakopitia,
Balaa ikawa baa, nayo Armageddonia,
Dini pasi kuongoza, yazuka maangamizi!

Si lazima ninajua, siasa kuziingia,
HIzi zinao udhia, wenyewe kuwaachia,
Wanasiasa wakawa, mkaa wajipalia,
Dini pasi kuongoza, yazuka maangamizi!

Mimbari kuzitumia, kaumu kuiokoa,
Kwa hadhari kuitoa, na mabaya kufichua,
Siri zitatuumbua, Jahanamu kutuvaa,
Dini pasi kuongoza, yazuka maangamizi!

No comments: