Saturday, March 24, 2012

Peperushwa

Hadhi ikija kushushwa, walipo sipo walipo,
Adhama hujaamishwa, maana sasa mkopo,
Kila wanapotingishwa, kelele yao makopo,
Watakuja peperushwa, kama vumbi na upepo!

Ngazi ukishakushushwa, kama upo ni haupo,
Heshima utaishiwa, kibaki chako kiapo,
Na mengine yatazushwa, ukajageuzwa dampo,
Watakuja peperushwa, kama vumbi na upepo!

Halali huharamishwa, iishie ufikapo,
Yaliyofichwa huamshwa, yakadaiwa malipo,
Hufufuka yalofishwa, lisilopo, likawepo,
Watakuja peperushwa, kama vumbi na upepo!

Wasio nguo huvishwa,hata mabawa ya popo,
Hujaliwa kilichoisha, na wala si kilichopo,
Huja yaliyopeperushwa, yakiletwa na upepo,
Watakuja peperushwa, kama vumbi na upepo!

Kwingine yataanzishwa, kila aina majopo,
Watu wakakutanishwa, kuzungumza yasiyopo,
Bendera zikaja shushwa, waondoke waliopo,
Watakuja peperushwa, kama vumbi na upepo!

Na wengine huja shushwa, wa mwiko kuwa mkopo,
Hupakuliwa vikesha,aidha papo kwa hapo,
Hutoa na kujumlishwa, walioko, wasiopo,
Watakuja peperushwa, kama vumbi na upepo!

No comments: