Monday, March 26, 2012

Radhi asiyekuomba

MUNGWANA akikosea, mwepesi kujikosoa,
Kitu anajidhania, na ubora kajitia,
Vyema kumuangalia, mwalimu wake dunia,
Radhi asiyekuomba, dharau huyo kajaa.

Yeye anakukosea, ujeuri ajitia,
Kisha akunyanyapaa, mithili una hatia,
Kwa dharau ashupaa, na vijembe kuvitia,
Radhi asiyekuomba, dharau huyo kajaa.

Shetani keshamwingia, moto kamzawadia,
Damu inamchochea, na hasira kumjaa,
Ubaya afrikira, anapokuangalia,
Radhi asiyekuomba, dharau huyo kajaa.

Unafiki amejaa, nje awachangamkia,
Na umbeya augawa, kusema ameonewa,
Ukweli wanaojua, haweshi kumshangaa,
Radhi asiyekuomba, dharau huyo kajaa.

Ukweli huukimbia, uongo kushikilia,
La ajabu hurudia, kama anakutania,
Kimya budi kukaa, iko siku atavia,
Radhi asiyekuomba, dharau huyo kajaa.

Mjinga hukudhania, unavyomvumilia,
Siri hajaitang'amua, bado anakuchezea,
Mwenye imani hujua, na subira huwania,
Radhi asiyekuomba, dharau huyo kajaa.

Naye huzidi mwombea, amnusuru Jalia,
Hisani humfanyia, japa hayawani kawa,
Nafsi huililia, shetani kumuingia,
Radhi asiyekuomba, dharau huyo kajaa.

Mengi huyafikiria, mazuri yaliyokuwa,
Wana kutowasumbua, ambao hawajakuwa,
Muda akajiwekea, wana wapate kukua,
Radhi asiyekuomba, dharau huyo kajaa.

Ahali huzingatia, yao wote majaliwa,
Ukweli akiujua, hupuuza yalokuwa,
Moja akaliangalia, la wote linalowafaa,
Radhi asiyekuomba, dharau huyo kajaa.

Mhanga hujitolea, au kafara akawa,
Bora apare kuzua, nusura ikawafaa,
Na wanaojitambua, ukweli wakaujua,
Radhi asiyekuomba, dharau huyo kajaa.

Mwisho nimeshafikia, kalamu naiachia,
Heri wanaosikia, uzima watajaliwa,
Ole wao wasojua, mauti yawavizia,
Radhi asiyekuomba, dharau huyo kajaa.

No comments: