Saturday, March 10, 2012

Kwa hicho unachokula

Haki kujihakikishia, kuuliza inafaa,
Kwa hicho unachopewa, wananchi unawafaa,
Kama unapewa mia, yepo kwao manufaa,
Kwa hicho unachokula, wananchi wapata nini?

Milioni ukipewa, kwa njia ipi wazua,
Mambo yenye kuwafaa, unaowahudumia,
Chini uwe wawatoa, juu wapate kuingia?
Kwa hicho unachokula, wananchi wapata nini?

Mipango ukipangia, bora kweli inakuwa,
Au yawa ni sanaa, akili kuwachezea,
Miaka kujiishia, maktaimu wawatia?
Kwa hicho unachokula, wananchi wapata nini?

Tazameni Malaysia, wao walivyoazimia,
Mishahara kukataa, hadi watu kunyanyua,
Hadi nchi ilipopaa, ndio wakajikumbukia,
Kwa hicho unachokula, wananchi wapata nini?

Hapa twataka pokea, huduma bila kutoa,
Kisha tukajilimbikia, watu wanavyogaiwa,
Vyao tukavichukua, vya kwetu tukajitia,
Kwa hicho unachokula, wananchi wapata nini?

Nchi inateketea, kwa dhuluma kuzilea,
Eti twajali sheria, huku watu waibiwa,
Kiatu changu navua, nisije kuwatupia,
Kwa hicho unachokula, wananchi wapata nini?

Naona ni ukichaa, nami nisiwe kichaa,
Hukumu namuachia, wote anayetujua,
Aje kuwaangazia, nyie na kizazi pia,
Kwa hicho unachokula, wananchi wapata nini?

Haki haitapotea, kwa dhuluma mkijitia,
Hakimu kabarikiwa, ni mjuzi alokuwa,
Hahitaji kuambiwa, kila kitu anajua,
Kwa hicho unachokula, wananchi wapata nini?

No comments: