Monday, March 26, 2012

Mwana mpotevu

Wasojua biblia, mpotevu humwambaa,
Hali kitabu chajua, hadithi kimesimulia,
Kondoo aliyepotea, bora kuliko ya mia,
Mwana akiwa jeuri, akaja kuwa mzuri,
Akesha wake ubishi
Wazazi kuwasikia,
Wazee hujivunia
Na radhi kumuachia!

Ni wale wenye nizaa, hiyana na kuchukia,
Mwana watamuachia, imuadhibu dunia,
Na motoni huingia, kwakushindwa kumlea,
Mwana akiwa jeuri, akaja kuwa mzuri,
Akesha wake ubishi
Wazazi kuwasikia,
Wazee hujivunia
Na radhi kumuachia!

Nusura haitakuwa, mwana akishapotea,
Imelani biblia, nasisi twaisikia,
Ila kwa wenye tamaa, yao yakatengenea,
Mwana akiwa jeuri, akaja kuwa mzuri,
Akesha wake ubishi
Wazazi kuwasikia,
Wazee hujivunia
Na radhi kumuachia!

Mwana aliyelelewa, wazazi awasikia,
Ukubwani huja via, akawa sana mbaya,
Au taahira kuwa, kimya ajinyamazia,
Mwana akiwa jeuri, akaja kuwa mzuri,
Akesha wake ubishi
Wazazi kuwasikia,
Wazee hujivunia
Na radhi kumuachia!

Wazazi humfanyia, kila hali kila njia,
Naye si wa kupigania, bali wa kupiganiwa,
Hupewalo huchukua, akosacho huachia,
Mwana akiwa jeuri, akaja kuwa mzuri,
Akesha wake ubishi
Wazazi kuwasikia,
Wazee hujivunia
Na radhi kumuachia!

Vijana wanatakiwa, watundu waliokuwa,
Wazee wamepotea, dhambi wameziachia,
Wengi wajisaidia, na si wa kusaidiwa,
Mwana akiwa jeuri, akaja kuwa mzuri,
Akesha wake ubishi
Wazazi kuwasikia,
Wazee hujivunia
Na radhi kumuachia!

Mali wajilimbikia, kushoto pia kulia,
Vyeo wavigombea, hata kwa wasiyoyajua,
Nchi watuharibia, kwa rushwa kuzipokea,
Mwana akiwa jeuri, akaja kuwa mzuri,
Akesha wake ubishi
Wazazi kuwasikia,
Wazee hujivunia
Na radhi kumuachia!

Watoto wa kufikia, kazi wanagawiwa,
Madudu watufanyia, wawalinda kwa hatia,
Kizungumkuti ubia, walokwisha wawafaa,
Mwana akiwa jeuri, akaja kuwa mzuri,
Akesha wake ubishi
Wazazi kuwasikia,
Wazee hujivunia
Na radhi kumuachia!

Taahira walokuwa, wengine waheshimiwa,
Huku wakijabomoa, kule wanahamishiwa,
Nasi tumeyang'amua, ulizo twawaachia,
Mwana akiwa jeuri, akaja kuwa mzuri,
Akesha wake ubishi
Wazazi kuwasikia,
Wazee hujivunia
Na radhi kumuachia!

Ni nje kiteknolojia, akili wanachezewa,
Wabaki kung'amg'ania, kumbe wanaporomoa,
Waiza demokrasia,kumbe ndio wajiua,
Mwana akiwa jeuri, akaja kuwa mzuri,
Akesha wake ubishi
Wazazi kuwasikia,
Wazee hujivunia
Na radhi kumuachia!

Fakiri tulokuwa, haramu twageuziwa,
Kidogo chanyakuliwa, watoto wao kupewa,
Huwa kama vile kawa, patupu ukifunua,
Mwana akiwa jeuri, akaja kuwa mzuri,
Akesha wake ubishi
Wazazi kuwasikia,
Wazee hujivunia
Na radhi kumuachia!

Karima twamlilia, wajawe kutuhurumia,
Na wanaotunyanyapaa, riziki yao kuvia,
Ulinzi ukautoa, uchi wapate bakia,
Mwana akiwa jeuri, akaja kuwa mzuri,
Akesha wake ubishi
Wazazi kuwasikia,
Wazee hujivunia
Na radhi kumuachia!

No comments: