Sunday, March 4, 2012

Ni kwenye jivu la moto

Bila moto kuenea, uchome yasiyokuwa,
Mwishowe majivu kuwa, na chini yakasambaa,
Na pindi yanapokuwa, mbegu mpya huchipua,
Ni kwenye jivu la moto, mabadiliko huzuka!

Uongo ukizidia, na ukweli watakiwa,
Wema wasipozaliwa, uovu huendelea,
Shetani akashangilia, nchi ameishikilia,
Ni kwenye jivu la moto, mabadiliko huzuka!

Dini wanaotumia, watu wetu kuwagawa,
Shimoni wasipochimbiwa, watalileta balaa,
Nasi tukiwavumilia, hukumu tunaitoa,
Ni kwenye jivu la moto, mabadiliko huzuka!

Hukumu tunaitoa, nchi hii kulaniwa,
Kwayo yatakayotokea, kizazi kitachoingia,
Hakuna wa kujitoa, dhambini tutaingia,
Ni kwenye jivu la moto, mabadiliko huzuka!

Wezi wanapoachiwa, wengine kuwaibia,
Ya kwao yakawafaa, na kisha wakasifiwa,
Na heshima wakapewa, kwa msingi wa nazaa,
Ni kwenye jivu la moto, mabadiliko huzuka!

Dhuluma ikichanua, watu hadi kulemaa,
Hulipuka wenye nia, moto unaojitambua,
Kila pahali kwingia, hata panapozuiwa,
Ni kwenye jivu la moto, mabadiliko huzuka!

Jivu linapobakia, mashaka nao ukiwa,
Watoto wanapolia, wanawake kugugumia,
Nchi hushtuliwa, na vilio na ukiwa,
Ni kwenye jivu la moto, mabadiliko huzuka!

Ni nani wa kuongoa, nchi inayopotea,
Mabaya kuyazuia, yanayotunyemelea,
Bila Rabi kumuingia, na kisha kumuangukia?
Ni kwenye jivu la moto, mabadiliko huzuka!

No comments: