Monday, March 26, 2012

Mguu mmekosea

Wenzangu nawausia, marafiki kuchagua,
Wapo tunaowajua, utumwa walitutia,
Na ubaguzi wajaa, kwao bado ni kadhia,
Historia yatwambia, mguu umeshakosea!

Historia twaijua, milango twawaachia,
Na bado twajionea, waipondavyo dunia,
Askari wamekuwa, ukubwa wameukwaa,
Historia yatwambia, mguu umeshakosea!

Yao yanadidimia, nini watatupatia,
Ila kondomu kupewa, tena zilizochakaa,
Na za bure chandalau, eti dawa ya malaria,
Historia yatwambia, mguu umeshakosea!

Unafiki twajitia, hawa kuwavumilia,
Mugabe namchukia, ila kwa hili radhia,
Mashariki inafaa, sote tuanze elekea,
Historia yatwambia, mguu umeshakosea!

Nchi wanaigawa, ubaguzi warejea,
Elimu yao yapwaya, uhuni umeingia,
Na fedha zimepungua, raha zao ni karaha,
Historia yatwambia, mguu umeshakosea!

Wameacha mhofia, mmiliki wa dunia,
Ya watu yawazuzua, Usodoma waridhia,
Rafiki nao tukiwa, dhambi tunajibebea,
Historia yatwambia, mguu umeshakosea!

Watu ovyo wanaua, na sisi wao wabia?
Mola kumuhofia, wenzangu nawaambia,
Dhulumati hana njia, akhera nayo dunia,
Historia yatwambia, mguu umeshakosea!

Najua mwanichukia, ukweli ninapotoa,
Manjumati mmepewa, na makombo mwatumia,
Hayo yenu yawafaa, na sio sisi raia,
Historia yatwambia, mguu umeshakosea!

Utumwa mnatutia, kulekule mwarejea,
Ardhi mwagaiwa, bure vito kuchukua,
Pipi mkishazipewa, hayo yote mwaridhia,
Historia yatwambia, mguu umeshakosea!

Shahidi historia, itakavyowaumbua,
Dhalimu tutawajua, rahisi wanunuliwa,
Laana kuwaachia, wao na kizazi pia,
Historia yatwambia, mguu umeshakosea!

Yarabi twakuangukia, zahama kuiondoa,
Mapema itavyokuwa, kadri ukikadiria,
Nchi isije ungua, na watu kuteketea,
Historia yatwambia, mguu umeshakosea!

No comments: