Tuesday, March 27, 2012

MALI

Ukombozi kuchelewa, bado hatujajikomboa,
Miaka ikiyoyomea, subira nayo hupaa,
Na juu wanaokua, kuamsha watakiwa,
Mali wanatuambia, a lutta continua!

Huwezi juu kukaa, na kisha ukashangaa,
Na akili kulemaa, ni lipi la kuamua,
Watu wanakungojea, si wewe kuwangojea,
Mali wanatuambia, a lutta continua!

Vinatakiwa vifaa, raia kuwapatia,
Kazi wakazitambua, na nchi kuendlea,
Zana zinapopunguwa, majungu mwajitakia,
Mali wanatuambia, a lutta continua!

Na wale wenye tamaa, nafasi waingojea,
Kwa klila anayesinzia, sharti kuchomolewa,
Ukiamka ukalia, watu hukupuuzia,
Mali wanatuambia, a lutta continua!

Kizingiti ukishakua, watu budi kukung'oa,
Ndivyo ilivyo dunia, hili huwezi kimbia,
Inafaa kuchukua, hatua zinazofaa,
Mali wanatuambia, a lutta continua!

Kila aliye na njaa, katu hawezi tulia,
Hadi tumbo likajaa, na kiu kujinasua,
Haya usipoyatambua, wengi watakusumbua,
Mali wanatuambia, a lutta continua!

Na viziwi wahofiwa, haya kutoyasikia,
Na vipofu nao pia, wenda hawatajionea,
Ila waliochaguliwa, katika siku radhia,
Mali wanatuambia, a lutta continua!

Mambo si kuyangojea, ila kuyafuatilia,
Na kisha kuyachungua, ukweli ukaujua,
Halafu kuazimia, hatua ukachukua,
Mali wanatuambia, a lutta continua!

Afrika inalia, njie tumeshapotea,
Wengi twaigilizia, asili twaiachia,
Nako tunakoelekea, siko tunakotakiwa,
Mali wanatuambia, a lutta continua!

No comments: