Tuesday, March 6, 2012

Shanga zangu kiunoni

Yamenikuta jamani, nikiwa usingizini,
Godoroni si ndotoni, mwilini nimebaini,
Shanga zangu sizioni, zilokuwa kiunoni,
Shanga zangu kiunoni, nimeamka sizioni!

Hazikuwa kiunoni, mwenyewe nikajidhani,
Nikalola kibetoni, humo amo sizioni,
Nikashusha vitu chini, kitandani sizioni,
Shanga zangu kiunoni, nimeamka sizioni!

Labda ziko hapa chini, nikafanza kuamini,
Kutazama uvunguni, hata sindano sioni,
Nikajishika kichwani, pengine kuna utani,
Shanga zangu kiunoni, nimeamka sizioni!

Nilizivaa jioni, nilipotoka bafuni,
Nikatazama makini, kasoro niibaini,
Kiuno zilisakini, hapakuwa yumkini,
Shanga zangu kiunoni, nimeamka sizioni!

Nani afanya utani, nikajitia shakani,
Peke yangu niko ndani, zitokaje kiunoni,
Zimeyeyuka yakini, naamii sizioni,
Shanga zangu kiunoni, nimeamka sizioni!

Huu ni uchawi gani, dalili mbona sioni,
Papabawa huyu nani, asinigande mwilini,
Na kama akiwa jini, awe ni wa dini gani ?
Shanga zangu kiunoni, nimeamka sizioni!

Shanga hazina thamani, ila mwangu kiunoni,
Kaweka mahala gani, aipate raha gani?
Maji Marefu yamini, nambie ni kitu gani?
Shanga zangu kiunoni, nimeamka sizioni!

No comments: