Sunday, March 4, 2012

Huwezi danganya wote

Wajinga waliokuwa, leo macho wafunguliwa,
Ni bure kutarajia, ujingani kurudia,
Uongo wanaozua, matope wajipakaa,
Huwezi danganya wote, kote na wakati wote!

Vigumu nakuambia, ujinga kuurudia,
Wajinga waliokuwa, ukweli wakiujua,
Kapuni hutowatia, kwa uongo na hadaa,
Huwezi danganya wote, kote na wakati wote!

Hesabu watazijua, ulizowavurugia,
Jumla hawataitoa, na toa kutoongezea,
Wewe ukiwagawanyia, wao watakuzidishia,
Huwezi danganya wote, kote na wakati wote!

Gizani waliokuwa, mwanga ukiingia,
Hawawezi kutulia, nuru watashangilia,
Na chanzo kukigundua,wafanze yanayofaa,
Huwezi danganya wote, kote na wakati wote!

Ndani waliofungiwa, nje ukishawatoa,
Vigumu itakuwia, ndani tena kufundia,
Hilo watalikataa, na zahama kuizua,
Huwezi danganya wote, kote na wakati wote!

Vipofu waliokuwa, ghafla wakajaliwa,
Wakaona yalokuwa, na jinsi yalivyokuwa,
Upofu watakataa, wataitaka dunia,
Huwezi danganya wote, kote na wakati wote!

Ndivyo inavyotokea, katika hii dunia,
Sauti walozuiwa, punde juu zikitokea,
Ngurumo kubwa hupaa, kwnye anga za dunia,
Huwezi danganya wote, kote na wakati wote!

Husambaratika pwaa, uongo waliolaniwa,
Ya kwao kudhihakiwa,na wao kusimbuliwa,
Pasiwe wanapokaa,bila ya kukodolewa,
Huwezi danganya wote, kote na wakati wote!

Mola wasiomjua, hili hawatalijua,
Waweza kuendelea, na yao yaliyokuwa,
Ila siku yawajia, na haya watayajua,
Huwezi danganya wote, kote na wakati wote!

No comments: