Sunday, March 4, 2012

NCHI HUWA NANIHII

UKIZIDI usanii, nchi huwa nanihii,
Ikawa haina rai, yakabaki majidai,
Mvaa huwa havai, watu wakamkinai,
Nchi huwa nanihii, ukizidi usanii!

Hawangoji staftahi, kuukimbiza uhai,
Ya juu hawayajui, chini wanatanabahi,
Hashtuki mwenye ndui, mkoma akisabahi,
Nchi huwa nanihii, ukizidi usanii!

Kuna walioko hai, pia walioko hoi,
Hachanganyi goigoi, na kwenda mbio hajui,
Baadhi haitufai, kwa filimbi pia nai,
Nchi huwa nanihii, ukizidi usanii!

Hufunga mwenye kikoi, vyema, ovyo hajikwai,
Hueleka matlai, magharibi isiposwihi,
Mtambuzi hatambui, kama kitu hatumbui,
Nchi huwa nanihii, ukizidi usanii!

Mengine ni makuruhi, kusemwa haijawahi,
Hatorushika nishai, nje asiyejidai,
Hawajui, hawamjui, hii ndiyo yake rai,
Nchi huwa nanihii, ukizidi usanii!

Maisha ni utalii, na wote huwastahi,
Safari yake hajui, wa kumfaa uhai,
Hadharau, hakinai, ukarimu halaghai,
Nchi huwa nanihii, ukizidi usanii!

Naitazama jamii, ilozidi usanii,
Ucheshi na ulaghai, wakawa wayastahi,
Kamwe wasiojirai, kuutukuza uhai,
Nchi huwa nanihii, ukizidi usanii!

Na wengi hawajijui, wala hawajitambui,
Njaa inawalaghai, dhambi kudhani uhai,
Na hili silishangai, subira hawastahi,
Nchi huwa nanihii, ukizidi usanii!

No comments: