Friday, November 4, 2011

Ukubwa

Nautafuta ubwabwa, ni wapi nitaupata,
Ninaogopa majibwa, kuja nje kuning'ata,
Na vibaka kujakabwa, hawa ni watu matata,
Ukubwa nitaupata, tungo zikinukuliwa!

Siutafuti ukubwa, siwezi nikatakata,
Sikuzoea kubebwa, ninaridhika kudata,
Cheo kwangu si ukubwa, ni adili kuifata,
Ukubwa nitaupata, tungo zikinukuliwa!

Ukubwa nyumba ya gamba, kujivua nitajuta,
Kinanitosha kihamba, kwa miaka nikanata,
Kwa dhambi siwezi tamba, jahanamu sijapita,
Ukubwa nitaupata, tungo zikinukuliwa!

Ukubwa shamba la pumba, mabua wakeketa,
Si shangazi si mjomba, wote huwa watafuta,
Na ndugu wasioomba, sijawahi kuwakuta,
Ukubwa nitaupata, tungo zikinukuliwa!

Ukubwa nitaupata, tungo zikinukuliwa!

Ninahofia kukumbwa, na kichaa cha kusita,
Na hata ningeliombwa, ninglikataa mkata,
Majini nisije kumbwa, mitaani nikipita,
Ukubwa nitaupata, tungo zikinukuliwa!

Sitafuti kuja lambwa, miguu isiyotakata,
Kuja mgongo kuwambwa, kwa chupa yenye mafuta,
Komba akiwa mkombwa, vilimilimi humsuta,
Ukubwa nitaupata, tungo zikinukuliwa!

Wakubwa wazidi chambwa, ukubwani kutakata,
Nepi zote toboa tobwa, humo mikojo hupita,
Mwana asipoziribwa, mazoea huyafata,
Ukubwa nitaupata, tungo zikinukuliwa!

Kwazo tungo nimebambwa, na siwezi kuziwata,
Ugonjwa huwa nakumbwa, mistari wakifuta,
Ni kokoto sio mwamba, bahati sijaipata,
Ukubwa nitaupata, tungo zikinukuliwa!

Madhali nimeshaumbwa, ninayo yangu talanta,
HIli halina kugombwa, inshallah hufata,
Na vyote huweza kombwa, ila hili ni amana,
Ukubwa nitaupata, tungo zikinukuliwa!

Mwali bado sijapambwa, na mahari sijapata,
Washairi mnaombwa, shughuli kuja iteta,
Viwango wakavibamba, na hadhi kuipakata,
Ukubwa nitaupata, tungo zikinukuliwa!

Wasomaji wa kuimba, nyuma nao kufuata,
Pasiwe na wa kumchimba,wala goli la matuta,
Ili nikija kuimbwa, pasiwepo na utata,
Ukubwa nitaupata, tungo zikinukuliwa!

No comments: