Thursday, November 3, 2011

Malezi ya msahafu

Nipe yasiyokanushika, maneno ya ushairi,
Kwa aya nilizozishika, kusoma na kukariri,
Busara iliyojengeka, pasiwe wa kuhasiri,
Malezi ya msahafu,kweli na uadilifu.

Mimi dhaifu hakika, achia mbali fahari,
Kwa jina sikuzalika, unanipwaya urari,
Sio wa kutamanika, kwani sivai hariri,
Malezi ya msahafu,kweli na uadilifu.

Si mtu wa kutajika, darajangu ushairi,
Kiumbe wa kupukutika, matawini naghairi,
Huwezi juu niweka, chini yangu minghairi,
Malezi ya msahafu,kweli na uadilifu.

Kwalo nimeneemeka, mtoto wa mafakiri,
Uzawa ninaushika, wala kwalo sitahayari,
Ndiko nilikozalika, kwangu heri sio shairi,
Malezi ya msahafu,kweli na uadilifu.

Nje nilikwishafika, ninshavuka bahari,
Mabonde nilishavuka, na milima kuabiri,
Na hapo nilipofika, naona bado pazuri,
Malezi ya msahafu,kweli na uadilifu.

Naishi nisikotaka, wajibu natahadhari,
Nafanya nisiyotaka, kwa kuwa yana kheri,
Nateta nisiotaka, ili kupima urari,
Malezi ya msahafu,kweli na uadilifu.

Yangu yangefahamika, yakwa mambo dhahiri,
Vyema ningeeleweka, kwa fakiri na tajiri,
Ususi ninaosuka, usiwe na ujabari,
Malezi ya msahafu,kweli na uadilifu.

Nafasi ningeishika, nisingekuwa tajiri,
Ufalme ungenivuka, ningelipewa kasri,
Ushujaa nisingetaka, ningepewa uaskari,
Malezi ya msahafu,kweli na uadilifu.

Namshukuru Rabuka, mtajika yaa Dhari,
Dhara haikunifika, ila iliyo na kheri,
Na kizazi kakishika, siratul kusafiri,
Malezi ya msahafu,kweli na uadilifu.

Kitambo nilichofika, ni zaidi ya bukheri,
Malengo yaliyotimika, siwezi kuyakariri,
Na leo nikitimka, radhi ni yake Qahari,
Malezi ya msahafu,kweli na uadilifu.

No comments: