Kumekucha asubuhi, hayatokuwa ya jana,
Mapya tunasabahi, mbadala muamana,
Na walio bado hai, wazidi kutafutana,
Siasa za ulaghai,hazina nafasi tena.
Siasa za ulaghai, hazina nafasi tena,
Wananchi wanakinai, tena kwa mbio sana,
Uarabuni wadai, na Ulaya watafutana,
Siasa za ulaghai,hazina nafasi tena.
Uongo hauna rai, njia yake fupi sana,
Haki wajua kudai, lakini hauna amana,
Na wanaotanabahi, gamba hujivua sana,
Siasa kwangu si nai, filimbi zenye hiana,
Na wala haziwi tui, kwenye wali kumimina,
Na nazi jama hailiwi, bali huwa twatafuna,
Siasa za ulaghai,hazina nafasi tena.
Ulaghai haufai, dunia sio ya jana,
Na jambo halitokei, simu zaanza pishana,
Na kamera ziko hai, picha zitapatikana,
Siasa za ulaghai,hazina nafasi tena.
Facebook na anwai, nazo kukimbizana,
Kila kitu utawahi, watu kuhabarishana,
Siri kuficha huwahi, duniani utaziona,
Siasa za ulaghai,hazina nafasi tena.
Siasa za ulaghai, soma nazo kuachana,
Mustakabali tanabahi, ni watu kuaminiana,
Na hoja kutokinai, hadi kweli kupatikana,
Siasa za ulaghai,hazina nafasi tena.
Ni feli ya vurumai, haina kuelewana,
Watu huwa kama tai, angani kuraruana,
Na viranja goigoi, walifurahia sana,
Siasa za ulaghai,hazina nafasi tena.
Uhuru hauna bei, hata kama twapishana,
Hao wanaojidai, hawaijui laana,
Nashangaa istilahi, wafanza kujua sana,
Siasa za ulaghai,hazina nafasi tena.
Si rafiki si adui, hakuna mwenye dhamana,
Msiba kama kikoi, wote hujapokezana,
Na mbwani hatuwang'oi, naona ubishi sana,
Siasa za ulaghai, hazina nafasi tena.
Thursday, November 3, 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment