Friday, November 4, 2011

Baidhati

Wanihoji ya binati, moyo aliyenivaa,
Alikuwa ni wa kati, si mdogo si wa kujaa,
Alikuwa katikati, kama kimo cha Drogbaa,
Alikuwa baidhati, mithliye urulaini.

Machoye ya alizeti, kama saba yake pua,
Na usoye wa manati, masikio ya hidaya,
Mdomoye wa karoti, na nyusi za kusinzia,
Alikuwa baidhati, mithliye urulaini.

Umbole kama sketi, si dera wala gunia,
Kifua chake taiti, dodo zimetokezea,
Na nyigu hana pointi, kiuno kilivyokuwa,
Alikuwa baidhati, mithliye urulaini.

Mikono yake maskati, vidole vya kuumua,
Kucha zake kama nati, na bolti ziizovaa,
Kiwambo cha biskuti, hamu kinavyokutia,
Alikuwa baidhati, mithliye urulaini.

Nilisema siyapati, moyo ukanikatalia,
Nilisema sipakuti, roho ikaninyanyua,
Nilisema siyafati, miguu ikatangulia,
Alikuwa baidhati, mithliye urulaini.

Nilisema hajileti, ndani nakuta kajaa,
Sio wavu si wavuti, chambo kimenichambua,
Kamba mboga na chapati, ndipo nilipovijua,
Alikuwa baidhati, mithliye urulaini.

Mvuto wa kalimati, na hatua za kupaua,
Sauti ya mwansiti, na vilango kupitia,
Bashasha ya vijisenti, na kpaa cha kupaua,
Alikuwa baidhati, mithliye urulaini.

Mnaleta hamleti, bado yeye kuijua,
Nyonyo haijawa titi, si ndama wa kukamua,
Wa kanzu si wa suti, wa kupewa, wa kupewa,
Alikuwa baidhati, mithliye urulaini.

Na saladi si fruti, njaa nisingeijua,
Nakukuta sikukuti, mwendo ni nyingi hatua,
Sijui chikeni pati, bali kicheni najua,
Alikuwa baidhati, mithliye urulaini.

Sikucheza kriketi, pauni ningezianua,
Nililipenda busati, na utamu naujua,
Mithili yake visheti, mengine ni tantabelua,
Alikuwa baidhati, mithliye urulaini.

No comments: