Chanzo wasioamua, yapaswayo amuliwa,
Kwa wakati unaofaa, na haki kutengenea,
Siasa wanaotumia, visingizio kadhaa,
'Siombe vita vibaya, chanzo wasioamua!
Waoga wa kuamua, shujaa wa kuongea,
Ujanja wanaotumia, mahala pasipofaa,
Na za mkato njia, watakaozitumia,
'Siombe vita vibaya, chanzo wasioamua!
Kadiri wasiojua, yatakiwa kugawiwa,
Ukiritimba kuzua, fikra unapoua,
Na mabavu kutumia, dhidi ya wao raia,
'Siombe vita vibaya, chanzo wasioamua!
Haambiliki balaa, hakuna wanalosikia,
Kaburi hujichimbia, huku wanajionea,
Na hutaka kuingia, na wale wanowafatia,
'Siombe vita vibaya, chanzo wasioamua!
Uwezo wasiokuwa, ila wingi wa tamaa,
Ukubwa wanaolilia, hata watu kuwaua,
Nafsi wasiojua, tayari kuangamia,
'Siombe vita vibaya, chanzo wasioamua!
Uchama wanaotumia, uhalali kujitia,
Wananchi kuwagawa, majinuni wasojua,
Na kisha kuwatumia, malengo yao kufikia,
'Siombe vita vibaya, chanzo wasioamua!
Ni watu walolaniwa, toka walipozaliwa,
Na Mola huwasaidia, motoni kuja ingia,
Na laiti walingejua,ukubwa wangeukataa,
'Siombe vita vibaya, chanzo wasioamua!
Mamlaka wasoachia,pale wanapotakiwa,
Wakatafuta wabaya,kumbe wao ndo wabaya,
Bahaluli kutumia, mauti kuyaandaa,
'Siombe vita vibaya, chanzo wasioamua!
Katiba wakiwambiwa, si wao kuiandaa,
Ulaghai wajitia, na kughushi washtakiwa,
Wawaacha wanasheria,wajifanya wanajua,
'Siombe vita vibaya, chanzo wasioamua!
Ufisadi waulea, na mafisadi radhia,
Kwa mali wakiwafaa, chamani na nyumbani pia,
Na aibu wala haya, vigumu kujionea,
'Siombe vita vibaya, chanzo wasioamua!
Ni watu wasosikia, sikio linalojifia,
Ushauri huambaa, mradi wakajifanyia,
Kilio kinachofatia, hakitawasumbua,
'Siombe vita vibaya, chanzo wasioamua!
Ni muda kujiandaa, vijana wa Tanzania,
Nchi wanaochezea, lazima kuwafichua,
Kizazi kinachofatia, amani kikailea,
'Siombe vita vibaya, chanzo wasioamua!
Saturday, November 5, 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment