Tuesday, November 1, 2011

Ndio waitwa waziri

Ninajua ni waziri, sijui wanipa nini,
Sijaliona la kheri, hali yangu maishani,
Wamiliki gari zuri, baiskeli sioni?
Ndio waitwa waziri, lakini umefanyani?

Unalo hekalu zuri, kibanda sijabaini,
Wala unachohiari, mimi nao mgagani,
Najiona ni kafiri, na wewe muuminini,
Ndio waitwa waziri, lakini umefanyani?

Mkeo ana fahari, mtaani na kijijini,
Kwangu anataksiri, kesho yake haioni,
Akili hazifikiri, wala macho hayaoni,
Ndio waitwa waziri, lakini umefanyani?

Mkubwa sina kiburi, ila ukweli nasaini,
Unajifanyia mazuri, hali yangu taabani,
Vipi nisione shari, na chuki mwangu moyoni?
Ndio waitwa waziri, lakini umefanyani?

Utume sijaabiri, kupata moyo laini,
N'na mtumba si hariri, hali hiyo si hisani,
Imani ninaghairi, na huruma siamini,
Ndio waitwa waziri, lakini umefanyani?

Malaysia safiri, mawaziri wathamini,
Hakuna mwenye sifuri, vijijini na mjini,
Na wote wana hadhari, viongozi waadhini,
Ndio waitwa waziri, lakini umefanyani?

Hawakuwa majibari, kulimbikiza kwa tani,
Nyuma walitakabari, wapande kwanza wa chini,
Nchi kupata utajiri, nao wakalamba auni,
Ndio waitwa waziri, lakini umefanyani?

Kiherehere na kihari, ni nyie wetu watani,
Kuja juu ni fahari, kama krimu ya jibini,
Upofu ukadhihiri, msikiapo maskini,
Ndio waitwa waziri, lakini umefanyani?

Nawalaani fakiri, kwani hamnithamini,
Mvune yalo na shari, ardhini na mbinguni,
Ila mkitahayari, dua ni ritadi uldini,
Ndio waitwa waziri, lakini umefanyani?

No comments: