Tuesday, November 1, 2011

Naam waitwa mbunge

Waema sasa king'eng'e, ubunge kuubaini,
Ila tungali vihongwe, tungali nyuma jimboni,
Maana toka utuhonge, hatujakwona aslani,
Na'am waitwa mbunge, jimbo limepata nini ?

Tumebaki na misonge, na udongo sakafuni,
Hauuziki mkonge, wala miwa na majani,
Hadi kwa pepo tupungwe, za siasa matawini,
Na'am waitwa mbunge, jimbo limepata nini ?

Hatukukuchagua mbunge, uwe wa televisheni,
Tulitaka utujenge, hapo kwetu kijijini,
Machungu yasitusonge, tuipate afuteni,
Na'am waitwa mbunge, jimbo limepata nini ?

Ni ahadi na mizengwe, sasa tunayabaini,
Umekuwa kama ng'e, kuuma huonekani,
Na dawa yataka tonge, na nchayo mkiani,
Na'am waitwa mbunge, jimbo limepata nini ?

Uliyoyaunda magenge, sasa ni ya wahuni,
Wamekuwa kama kenge, hatuendi tena mtoni,
Acha nduguzo waringe, sisi faida hatwoni,
Na'am waitwa mbunge, jimbo limepata nini ?

Twamngoja mwanawange, uje kwenda likizoni,
Na virago uvifunge, ukaishi zako mjini,
Tuache sisi tuchunge, mapori bila hayawani,
Na'am waitwa mbunge, jimbo limepata nini ?

No comments: