Thursday, November 3, 2011

Katiba ni ya raia

Wastahili raia, katiba yao kufuma,
Makundi na jumuia, kutoa zao kalima,
Nalo watakaloamua, lipate yake heshima,
Katiba ni ya raia, na sio jambo la chama.

Washikadau twajua, ndio tunao watazama,
Kila mdau kuteua, ni nani kumpa dhima,
Wajumbe tukawajua, majukumu kuwatuma,
Katiba ni ya raia, na sio jambo la chama.

Nchi haitaridhia, binafsi kujituma,
Ajenda kupenyezea, kujihami pia chama,
Malengo kujatimia, ya wengine yakakwama,
Katiba ni ya raia, na sio jambo la chama.

Hadidu zilizochaa, zitajaleta zahama,
Zitawafanya vichaa, vijana na watu wazima,
Nchi tutaipasua, na vitali kurindima,
Katiba ni ya raia, na sio jambo la chama.

Uchama ukiingia, tutaifanya dhuluma,
Wengine watachukia, na pabaya kujitoma,
Ni wenyewe tutalia, tukipuuza hekima,
Katiba ni ya raia, na sio jambo la chama.

Viongozi watambua, hawa ni watu adhama,
Ila njia wachagua, isiyo nayo heshima,
Wajinga watudhania, kwalo hatutawafuma,
Katiba ni ya raia, na sio jambo la chama.

Tumebobea sheria, hamsini twajituma,
Vipi kutozingatia, mabingwa wanayosema,
Wanasiasa wazua, za kipuuzi kalima,
Katiba ni ya raia, na sio jambo la chama.

Wanasiasa najua, ujuzi wanauazima,
Kile wanachoamua,, wameambiwa kusema,
Vipi katiba kutia, kisicho nayo rehema,
Katiba ni ya raia, na sio jambo la chama.

Mtunzi nawazindua, chama mwakataa pema,
Usononi mwaingia, na vidole vya tuhuma,
Mtakuja laumiwa, hadi kizazi kukoma,
Katiba ni ya raia, na sio jambo la chama.

Ninamuomba Karima, kikombe kukiepua,
Wachovu kuwaandama, mbali kupatilizia,
Nyuma kije kizazi chema, utu kinachotambua,
Katiba ni ya raia, na sio jambo la chama.

Tuepushe na maamuma, watokacho wasojua,
Tuepushe na dhuluma, nchi nayotufanyia,
Tuepushe na zahama, wabaya wanazotutakia,
Katiba ni ya raia, na sio jambo la chama.

No comments: