Haiwi kitu cha mtu, ni ya wananchi katiba,
Twamwambia kila mtu, toka mtoto na baba,
Katiba iwe ya watu, ili iwe marahaba,
Katiba ni ya wananchi, na sio kitu cha mtu.
Katiba sheria yetu, kwa tawala yenye tiba,
Hatukubali wenzetu, kuja ifanya ghiliba,
Watumie mali zetu, wakala hadi kushiba,
Katiba ni ya wananchi, na sio kitu cha mtu.
Hatukubali wenzetu, njaa yetu kuziriba,
Sisi pia na wenetu, tukaikosa nasaba,
Taabu maisha yetu, ikawa nayo mahaba,
Katiba ni ya wananchi, na sio kitu cha mtu.
Katiba katu si ya mtu, nyie hamli mkashiba,
Na katiba si viatu, na sisi tukawa raba,
Katiba haina kutu, sio chuma wala shaba,
Katiba ni ya wananchi, na sio kitu cha mtu.
Huu mkataba wetu, watawala kuubeba,
Wasifanye yaso utu, ama nasi tutagomba,
Tuchukue viti vyetu, tukishakuwakaba,
Katiba ni ya wananchi, na sio kitu cha mtu.
Katiba milki yetu, na sisi sio majuba,
Twastahili wenetu, kutengeneza ratiba,
Na majumuisho yetu, yakaifanya katiba,
Katiba ni ya wananchi, na sio kitu cha mtu.
Thursday, November 3, 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment