Thursday, November 3, 2011

Katiba yake rais

Ikiwa yake rais, katiba tunayotafuta,
Naona kuna nuksi, maafa itayaleta,
Itakuwa muflisi, tasa, gumba na utata,
Katiba yake rais, itampa udikteta.

Itakuwa ni najisi, tohara haitaileta,
Udhu kuwa na nakisi, japo wachache kupeta,
Nausia kadamnasi, katiba sio kuteta,
Katiba yake rais, itampa udikteta.

Katiba ni majilisi, hoja zinazotakata,
Zisizo ubinafsi, wala uchama kung'ata,
Haitaki wasiwasi, sintofahamu kukuta,
Katiba yake rais, itampa udikteta.

Katiba si wasiwasi, na mashaka kuyaleta,
Huandamwa na mikosi, na hata kuleta vita,
Yataka wema wasusi, usawa wanaopakata,
Katiba yake rais, itampa udikteta.

Tutakujaondoka sisi, na wengine kufuata,
Tukiacha makamasi, mikono itawanata,
Watakua kuyafosi, waishie mazezeta,
Katiba yake rais, itampa udikteta.

Katiba yake rais, umaskini huleta,
Mubarak muasisi, twajua yaliyomkuta,
Ukubwa si almasi, neema isiyolelta,
Katiba yake rais, itampa udikteta.

Katiba si wafuasi, ila raia kuteta,
Yaliyo na wasiwasi, hadharani kukung'ta,
Zulia nazo libasi, nje, ndani kutakata,
Katiba yake rais, itampa udikteta.

No comments: