Tuesday, November 1, 2011

Sikio linalokufa

Sikio linalokufa, kusikia mashakani,
Hata kabla ya kufa, sauti hazendi ndani,
Na pale linapokufa, uziwi ni maskani,
Sikio linalokufa, halitosikia dawa!

Sio mja sio khalifa, uziwi dhiki kiini,
Si spika wala bufa, kusikia si yumkini,
Hisia zawa kifafa, uelewa majinuni,
Sikio linalokufa, halitosikia dawa!

Usimwate kwa orofa, aweza anguka chini,
Mshushe kama wadhifa, hastahili makani,
Mkoa mpe tarafa, na kata aje mtaani,
Sikio linalokufa, halitosikia dawa!

Uongozi si sharifa, kwa wengine ni uhuni,
Hawaijui kaifa, na staha sio makini,
Msizingojee zafa, maandamano nchini,
Sikio linalokufa, halitosikia dawa!

Haijaniwia hanifa, nafuu yake sioni,
Sikio lililokufa, kuja valishwa miwani,
Haiyumkiniki latifa, namna hii kuauni,
Sikio linalokufa, halitosikia dawa!

Mengine kama kashfa, watoto huzibaini,
Halihitaji maarifa, akili mwako kichwani,
Dhara haina shufaa, kiranja usiitamani,
Sikio linalokufa, halitosikia dawa!

No comments: