Monday, October 31, 2011

Ukoloni wa mweusi

Wa weupe ukoloni, haukuwa wa kisasi,
Kumezuka majinuni, wa bakora na bisibisi,
Kuwapinga uhaini,watakujakutoa kamasi,
Ukoloni wa weusi, heri ya ule wa weupe!

Hujikweza kiutani, akaipita kamusi,
Maneno kwa dizaini, ni lukuki na fususi,
Na kumbe ni majinuni, nchi yapata nakisi,
Ukoloni wa weusi, heri ya ule wa weupe!

Mipango haubaini, ukoloni wa mweusi,
Mambo yenda kwa anwani, za ahali na watesi,
Hana anayemwamini, na mapya hawaasisi,
Ukoloni wa weusi, heri ya ule wa weupe!

Ungejua walakini, wakati unavyoasi,
Umdhaniye makini, kabeba zake nuksi,
Ya uani barazani, hawana siri wasusi,
Ukoloni wa weusi, heri ya ule wa weupe!

Mweupe alithamini, tasihili na wepesi,
Goigoi kuwahini, wasiwalete waasi,
Njia akazibaini, si kwa thuluthi na sudusi,
Ukoloni wa weusi, heri ya ule wa weupe!

Alihofu uyakini, hilo hakuwa mwepesi,
Aliyatia shakani, ambayo hakuakisi,
Hakuna aliyemwamini, hata mke na damisi,
Ukoloni wa weusi, heri ya ule wa weupe!

Kusoma aliamini, hakuacha kudurusi,
Kubahatisha mgeni, hilo hakutanafusi,
Kakataa usanii, kama hauna asasi,
Ukoloni wa weusi, heri ya ule wa weupe!

Na katika mitihani, hakutunyima maksi,
Kila aliye makini, haki kapewa kiasi,
Na pia wakashaini, washairi na watesi,
Ukoloni wa weusi, heri ya ule wa weupe!

Weusi kama utani, wazidi kwa ubinafsi,
Vya kwao huvithamini, na sio vya kadamnasi,
Kishenzi hujiamini, vigumu dhiki kuhisi,
Ukoloni wa weusi, heri ya ule wa weupe!

Wananchi wanshabaini, ukoloni wa mweusi,
Tofauti dizaini, atharize mahsusi,.
Kadhalika walakini, balaa pia mikosi,
Ukoloni wa weusi, heri ya ule wa weupe!

Niepushe aliamini, kwa hasira na kisasi,
Nipe adili auni, fukara au mkwasi,
Nikidhie tathmini, sheriazo nisiasi,
Ukoloni wa weusi, heri ya ule wa weupe!

Nikwepe uhayawani, nitese nisianisi,
Nijaze kheri kichwani, daima nisikuasi,
Nifanye mtu makini, kwa ushauri wa asasi,
Ukoloni wa weusi, heri ya ule wa weupe!

No comments: