Saturday, October 1, 2011

Utajiri si hoja, hata zuzu hutajirika!

Mjinga hutajirika, na mali kwake ikaja,
Hujenga kikajengeka, kishakikaja kuvuja,
Huzikwa pia mzika, sikuye naye ikija,
Utajiri si hoja, hata zuzu hutajirika!

Maisha ya watajika, hayaji kwa rejareja,
Yataka watu kusuka, kwa ibada nazo hija,
Na kutovuka mipaka, ya Mola alo mmoja,
Utajiri si hoja, hata zuzu hutajirika!

Matajiri huzuzuka, neema inapokuja,
Wakajiita Rabuka, ma wala si tena waja,
Huamini wakitaka, lolole lile kwao huja,
Utajiri si hoja, hata zuzu hutajirika!

Uzima sio shirika, haiji na haijaja,
Muumba hana shirika, sirize ngumu kuvuja,
Vigumu kueleweka, kumpa asiyemtaja,
Utajiri si hoja, hata zuzu hutajirika!

Dunia hii hakika, inatawala mirija,
Hujiona wastahika, kula mia sio moja,
Kulimbikiza hutaka, na sio kufunga mkaja,
Utajiri si hoja, hata zuzu hutajirika!

Watu hawa huibuka, kila awamu zikija,
Na kile wanachoweka, ni mtaji unaovuja,
Utawala kuupaka, kwa mafuta ya Unguja,
Utajiri si hoja, hata zuzu hutajirika!

Waaminiwao wahaka, wavaa la dhambi koja,
Na kila wanachokishika, Midasi ana faraja,
Na jipu likitumbuka,usaa hauachi kuvuja,
Utajiri si hoja, hata zuzu hutajirika!

Utajiri bila shaka, hakika sio kioja,
Yetu makubwa mashaka, ni kidari na mapaja,
Huo wao ushirika, nchi unaoifuja,
Utajiri si hoja, hata zuzu hutajirika!

Inatutia mashaka, zuzu naye kuwa na hoja,
Na weledi wakashika, toka kwake lau moja,
Na nchi ikafunguka, ukajaisha uteja,
Utajiri si hoja, hata zuzu hutajirika!

No comments: