Monday, October 31, 2011

Hudhalilika mjanja

Ukubwa wanaoonja, kuuacha hujikinga,
Huutafuta ujanja, vyeo vyao kuvizinga,
Hudiriki kuwapunja, wanaodhani wajinga,
Hudhalilika mjanja, akijifanya mjinga!

Wanazuka chinjachinja, mumiani wanawanga,
Utamu wanaoonja, kuukosa wanaganga,
Naona alama za denja, Kaole na Sumbawanga,
Hudhalilika mjanja, akijifanya mjinga!

Nchi ni chake kiwanja, cha nchi anayejenga,
Mwananchi havuti ganja, na huwezi kumfunga,
Akishakwa mjanja, hukukimbia waganga,
Hudhalilika mjanja, akijifanya mjinga!

Wazuka wapya viranja, wasaga kisha kutwanga,
Kina Mhina pia Minja, uchifu hamtawavunga,
Makabila yataanja, heshima yao kudunga,
Hudhalilika mjanja, akijifanya mjinga!

Msijifanye wajanja, wananchi wawe wajinga,
Miiko mshaivunja, sasa mwataka matanga,
Na nchi mwenye kuvunja, ni kiongozi mjinga,
Hudhalilika mjanja, akijifanya mjinga!

Hudhalilika mjanja, akiigiza ujinga,
Utajipakaje wanja, kama nisai kuringa,
Unauweza msanja, au wataka tuvunga?
Hudhalilika mjanja, akijifanya mjinga!

Nchi yaweza jikunja, na nyie ikawasonga,
Uongozi si ujanja, ila ni nchi kuiganga,
Enzi za wale wajanja, ukomo zimeshagonga,
Hudhalilika mjanja, akijifanya mjinga!

Wajua mimi si mjanja, mmiliki ardhi na anga,
Nachunga changu kiwanja, peponi unachojenga,
Huu mwiko sintavunja, na sihitaji ubingwa,
Hudhalilika mjanja, akijifanya mjinga!

Mimi mtu wa kubanja, nitawezaje kuringa,
Hali yangu ya ugonjwa, lipi kubwa nitajenga,
Mtu wa kuni kuchanja, ghorofa siwezi jenga,
Hudhalilika mjanja, akijifanya mjinga!

Watatafutwa na ninja, kuvurunda wakiganga,
Watageuzwa makanja, mafundi wa kuboronga,
Na mifumo watavunja, ahali wanaowakinga,
Hudhalilika mjanja, akijifanya mjinga!

No comments: