Tuesday, October 25, 2011

Hadhi yetu ni kaniki

Hakika hili sipati, wadhifa nikihakiki,
Mshairi siwasuti, na wala siwashtaki,
Naitafuta risiti, na kile mnachomiliki,
Mbona mnavaa suti, na hadhi yetu kaniki?

Hali yenu hatihati, mnavaa ya malaki,
Kuunganisha sikuti, mikono inshataliki,
Na majibu siyapati, ya haramu au haki,
Mbona mnavaa suti, na hadhi yetu kaniki?

Najua kuna tovuti, na redio mnamiliki,
Televisheni zi kati, na simu zinatamalaki,
Wastani hauleti, hesabu haihesabiki,
Mbona mnavaa suti, na hadhi yetu kaniki?

Ajabu kuvaa suti, na hadhi yetu kaniki,
Za kiume na sketi, wakwasi wataharuki,
Sijui ni utanashati, au unyani twadhihaki,
Mbona mnavaa suti, na hadhi yetu kaniki?

Ingekuwa shuruti, China isingeafiki,
Mandela angetroti, awe naye mnafiki,
Baridi ya afriti, Afrika haifiki,
Mbona mnavaa suti, na hadhi yetu kaniki?

Hainikwami sauti, tai sijaiafiki,
Nisingemimina beti, ila kwa sauti haivaliki,
Nikiwaza malimati, fakiri wasivyonaki,
Mbona mnavaa suti, na hadhi yetu kaniki?

Unafiki hauvuti, wengi kwenye halaiki,
Waona kama nishati, kuwepo haiaminiki,
Kwa wengi sanda ni suti, huvaa bila kumiliki,
Mbona mnavaa suti, na hadhi yetu kaniki?

Mtenzi nimetafiti, na hili sijabariki,
Tutafute ya bahati, mavazi yenye ashiki,
Waafrka tuketi,mila zetu tuhakiki,
Mbona mnavaa suti, na hadhi yetu kaniki?

Tubuni yetu mashati, na sarawili za kindaki,
Kinamama ni sketi, na magauni ya saki,
Hakimilki idhibiti, watuige Waturuki,
Mbona mnavaa suti, na hadhi yetu kaniki?

Ya Mswati ya Mswati, ya kwetu yanashtaki,
Taifa kujizatiti, desturi zitamalaki,
Zesha za kina waiti, zaja za chaki na cheki,
Mbona mnavaa suti, na hadhi yetu kaniki?

No comments: