Sunday, October 23, 2011

Vijana msigawanyike

Msigawinyike vijana, kitaifa msigawike,
Itakuwa ni laana, ya wazee wawatwike,
Yakwao wao ya jana, mbeleko sasa tweleke,
Vijana msigawike, kuweni kitu kimoja.

Wakati wao ujana, kwa uhuru utumike,
Katu hawakubaguana, mkoloni aondoke,
Wazawa kuaminiana, ilibidi lifanyike,
Vijana msigawike, kuweni kitu kimoja.

Uhuru ulipatikana, bendera ipeperuke,
Ilibidi kushikana, Mwingereza ang'atuke,
Vijana msigawike, kuweni kitu kimoja.

Leo tunayoyanena, uchumi uimarike,
Lazima kupatikana, uchumi uhuru wake,
Nasi tusipoungana, ni vigumu lifanyike,
Vijana msigawike, kuweni kitu kimoja.

Wazee wajanja sana, wataka tugawanyike,
Ili wahodhi ubwana, na sisi tudhalilike,
Wengine hawana wana, na ukubwa ndio mke,
Vijana msigawike, kuweni kitu kimoja.

Muamana wa kupona, nchi dia waiweke,
Miaka tena hawana, kwanini wasononeke?
Mtakaopotezana, ni nyie mzainike,
Vijana msigawike, kuweni kitu kimoja.

Baraza haraka sana, lazima sasa lizuke,
Kuunganisha vijana, na kila chama watoke,
Dira na yetu amana, nchi sasa ijengeke,
Vijana msigawike, kuweni kitu kimoja.

Mafisadi kuwabana, na wazee waondoke,
Hakuna kubabaishana, budi uchumi uumuke,
Na sote kuhimizana, maarifa yatumike,
Vijana msigawike, kuweni kitu kimoja.

Bidii kuchagizana, na juhudi ifanyike,
Na wengine kutafutana, vijana mshikemshike,
Amerika na Uchina, mambo bora yapangike,
Vijana msigawike, kuweni kitu kimoja.

Seychelles na Guyana, Brazili tuwashike,
India na Botswana, mifano tukaiteke,
Russia mpaka Ghana, mbinu twige tuchangamke,
Vijana msigawike, kuweni kitu kimoja.

Iwe ni mwiko vijana, na wazee mtumike,
Ili wao kugawana, nyara ovu wazisake,
Ni sharti kuwabana, sasa wasambaratike,
Vijana msigawike, kuweni kitu kimoja.

Chama mjue ni jina, linaweza lifutike,
Kulikoni kuja uana, vingine budi tuzike,
Umoja wetu amana, amani sote tutake,
Vijana msigawike, kuweni kitu kimoja.

Watanzania kuibiana, lazima tupige teke,
Hiki chanzo cha hazina, kwa mabaya yafanyike,
Ikawa twapatilizana, taifa liserereke,
Vijana msigawike, kuweni kitu kimoja.

Ili sote kuungana, maandamano tukoke,
Wazee kuja wabana, fungamano lifanyike,
Na kiapo kuapizana,vijana wasitumike,
Vijana msigawike, kuweni kitu kimoja.

Na kiapo kuapizana, vijana wasitumike,
Kuja sisi kutugawanya, na vita vije vizuke,
Kwa nia njema kuagana, nchi wenyewe tushike,
Vijana msigawike, kuweni kitu kimoja.

Namshukuru Rabana, umoja ausimike,
Na usiku na mchana, mipaka yetu ilindike,
Na uchumi kufaana, wote juu tunyanyuke,
Vijana msigawike, kuweni kitu kimoja.

No comments: