Sunday, October 23, 2011

Fisadi mvunja nchi

Hafai kuvumiliwa, fisadi hana rafiki,
Ubinafsi kajaa, vyote hutaka milki,
Mtaji hujipatia, kwa njia zisizo haki,
Fisadi hana rafiki, na hafai vumiliwa.

Kunyonga keshazoea, kuchinja hayumkiniki,
Za mkato kupitia, hizo njia amiliki,
Huwezi mtegemea, ni mkubwa mnafiki,
Fisadi hana rafiki, na hafai vumiliwa.

Ajua kuwatumia, bila malipo ya haki,
Mawazo huyachukua, akidai hayataki,
Kisha huja kutumia, kwa kuiba hatimilki,
Fisadi hana rafiki, na hafai vumiliwa.

Wakubwa huwahadaa, kama binti na Fataki,
Ajua kuwasifia, magharibi, mashariki,
Wakajiona wajua, kumbe bure mamluki,

Ni mabuzi atumia, kuwachuna pasi breki,
Na anavyozitumia, Mangi atamtaliki,
Hisia hufa kifua, ukubwa kutamalaki,
Fisadi hana rafiki, na hafai vumiliwa.

Mbumbumbu wangelikuwa, utadhani mabruki,
Si watu wa kuaminiwa, kawalaani Maliki,
Pepo hujitangazia, dunia itawashtaki,
Fisadi hana rafiki, na hafai vumiliwa.

Akili hawajatulia, utadhani mashabiki,
Huishi kwa kubabia,kwa dhuluma za riziki,
Muhali kuhesabiwa, kwani hawajumliki,
Fisadi hana rafiki, na hafai vumiliwa.

Kama ningeliwatambua, nawafanza mshikaki,
Wazi ningewachambua, niwachome kwa hamaki,
Wananchi kuwagawia,wale na wanywe na wiski,
Fisadi hana rafiki, na hafai vumiliwa.

Wanaojichukulia, taifa isivyo haki,
Kujimilikisha dia, nchi kuwa yao milki,
Wakawa waitumbua, mwananchi wamdhihaki,
Fisadi hana rafiki, na hafai vumiliwa.

Ardhi tunayokalia, hii ni ya kwetu haki,
Iweje kutuvamia, mkawa wastahiki,
Malipo kuyachukua, sisi tupu tukabaki?
Fisadi hana rafiki, na hafai vumiliwa.

Macho tumefunguliwa, tutaipigania haki,
Wawekezaji kujua, ardhi haikaliki,
Chetu tusipokujapewa, na hisa nazo kumiliki,
Fisadi hana rafiki, na hafai vumiliwa.

Tumechoka hadaiwa, hapa tena hatwondoki,
Dhahabu tutafukia, hadi malipo ya haki,
Ufukara twakataa, kijiji hakistahiki,
Fisadi hana rafiki, na hafai vumiliwa.

Kila atakeyingia, utajiri tutalaki,
Serikali kutwibia, katu haikubaliki,
Ni sisi tuliokaa, kijijini twastahiki,
Fisadi hana rafiki, na hafai vumiliwa.

No comments: