Tuesday, October 25, 2011

Sukari ashike nani

Hekima bila anwani, huishia ufukweni,
Na wapangaji makini, kubadili uhaini,
Mbele nyuma si auni, ni tabia ya kihuni
Sukari ashike nani, utamu aache nani?

Soko huru kubaini, vipi twavunja kanuni,
Twatafuta kitu gani,ili kumpendeza nani,
Rahisi si afueni, wakait mwingine duni,
Sukari ashike nani, utamu aache nani?

Mikoa twajizaini, kutawala kwa hisani,
Uhuru kuusaini, litapandisha mizani,
Ukiritimba kuwini, tutajikuta shakani,
Sukari ashike nani, utamu aache nani?

Utandawazi amini, mikoa huru yaghani,
Mipaka iwe laini, ya nje pia na ndani,
Na siasa kuzibuni, zisizo na walakini,
Sukari ashike nani, utamu aache nani?

Cha ndani hakipatikani, cha nje kiagizeni,
Soko lililo makini, linazijua kanuni,
Ukifuata mizani, hutokosa abadani,
Sukari ashike nani, utamu aache nani?

Mwataka ashike nani, sukari humu nchini,
Hivi kati yetu nani, utamu hauthamini,
Na hasa wa mamilioni, usoshika mikononi?
Sukari ashike nani, utamu aache nani?

Mbuzi ashike majani, ushahidi mashakani,
Viongozi hawaoni, au akili kichwani?
Nini wanchotumaini, kukipata ofisini?
Sukari ashike nani, utamu aache nani?

Ni shere yumkini, au mwatufanyia nini?
Mwahadaa watu gani, au walo afkani?
Ninacheka majinuni, hata mimi siamini
Sukari ashike nani, utamu aache nani?

Atashuka huku nani, aje aone ya chini,
Mwabakia ghorofani, hamjui ya ardhini,
Na uongo mwasaini, ukweli huku mwadhani,
Sukari ashike nani, utamu aache nani?

Kipanya haiwezekani, nyuma alishabaini,
Mwaumwa masikioni, dawa basi tafuteni?
Twajikuta hadharani, vigumu kuwatajeni,
Sukari ashike nani, utamu aache nani?

No comments: