Thursday, October 20, 2011

Mkosaji

Mbona kwake kawaida, mkosaji kupayuka,
Hii ni mila na ada, labda haijaeleweka,
Na ingelikuwa bida, tamaa isingejengeka,
Mkosaji kupayuka, ni jambo la kawaida.

Ni jambo la kawaida, mkosaji kupayuka,
Vitisho kwake kaida, mipaka hajaivuka,
Na kiada na ziada,
huagiza akitaka,
Mkosaji kupayuka, ni jambo la kawaida.

Kupayuka ni ibada, jua hilo kwa hakika,
Hata akienda eda, mengine hulalamika,
Utadhani kama buda, lakini aeleweka,
Mkosaji kupayuka, ni jambo la kawaida.

Kwake lisilo faida, manufaa hugeuka,
Na kileo akigida, maafa yakamfika,
Bado huwa kama nunda, kulalama kalogeka,
Mkosaji kupayuka, ni jambo la kawaida.

Watu wengine ni shida, hupati pa kuwaweka,
Hujichanganya mada, wakashindwa eleweka,
Ponda kugeuzwa poda,ni kipi utakachoshika?
Mkosaji kupayuka, ni jambo la kawaida.

No comments: