Sunday, October 23, 2011

Mwanademokrasia

Haogopi kuchukiwa, mwanademokrasia,
Kazi yake aijua,dhuluma huzikataa,
Dhulumati humuhadaa,Kama wao kujakua,
Mwanademokrasia, haogopi kuchukiwa.

Na asipowakubalia, huanza kumchukia,
Watamfanyia nazaa, kumzushia balaa,
Hata sumu huwekewa, uendelee ubaya,
Mwanademokrasia, haogopi kuchukiwa.

Siasa za kuhofia, wengi wau wana njaa,
Wengine wamebobea, matumbo yanavujia,
Hayawezekani kujaa, kila siku hupungua,
Mwanademokrasia, haogopi kuchukiwa.

Uchama naukataa, naijenga Tanzania,
Upande kutoegemea,ila demokrasia,
Nchi ipate kufaa,sio takataka kua,
Mwanademokrasia, haogopi kuchukiwa.

Nani kunisogelea, uongo naukataa,
Usanii nachukia, na dhuluma naijua,
Haki ninaililia, kila mtu Tanzania,
Mwanademokrasia, haogopi kuchukiwa.

Mapambano yaendelea, sasa uchumi hatua,
Umaskini kuuvua, huru kiuchumi kua,
Ikashindana mikoa, uchumi kuunyanyua,
Mwanademokrasia, haogopi kuchukiwa.

Siasa za kimatonya, mwisho sasa zafikia,
Chaja kizazi kipya, nchi kujaisimamia,
Nyuma wanaongalia, hapo hapo kubakia,
Mwanademokrasia, haogopi kuchukiwa.

Kazi nimeshairidhia, siwezi kuikataa,
Kuenzi demokrasia, hadi mizizi kukomaa,
Daima nitatetea, hadi kaburini kwingia,
Mwanademokrasia, haogopi kuchukiwa.

No comments: