Monday, October 31, 2011

Mapori bakini nayo

Wanyama 'wetu' twauza, mbaki nayo mapori,
Fedha twataka tengeza, hatuichezi kamari,
Hakuna wa kutuiza, hii ya hija safari,
Mapori bakini nayo, wanayama 'wetu; twauza!

Njaa inatuongoza, na wala si ujuzi,
Teua kilichooza, samadi ni matumizi,
Na mbwa naye ukicheza, masjidi fumanizi,
Mapori bakini nayo, wanayama 'wetu; twauza!

Kijani tumeagiza, ni rangi yetu ya kheri,
Dunia tunaijuza, kwetu heri huwa shari,
Uroho unatumaliza, na wala sio kiburi,
Mapori bakini nayo, wanayama 'wetu; twauza!

Hatukuja kutengeza, tumekuja kuathiri,
Nchi tutaigeuza, iwe kama harakiri,
Wenyewe mnajimaliza, kutimiza wetu urari,
Mapori bakini nayo, wanayama 'wetu; twauza!

Ahera tunawatanguliza, kuziepuka hatari,
Kadhalika kumaliza, gharika na ufakiri,
Kesho yenu twatengeza, hampaswi kufikiri,
Mapori bakini nayo, wanayama 'wetu; twauza!

Mwadhani mmetuweza, na sisi ni wajeuri,
Na sasa twawachuuza, kuupata utajiri,
Wazee tukishawatunza, huziondoa hatari,
Mapori bakini nayo, wanayama 'wetu; twauza!

Wazawa mate kumeza, hiyo ndiyo yao kheri,
Vyenu vyote twaviuza, na mkose ujasiri,
Mkishindwa kuyameza, kuna za bure safari,
Mapori bakini nayo, wanayama 'wetu; twauza!

Msisubiri mwangaza, kutakucha mghairi,
Na utu kutanguliza, mtajikuta washairi,
Twala na tunamaliza, ni nani mwenye jeuri?
Mapori bakini nayo, wanayama 'wetu; twauza!

No comments: