Sunday, October 23, 2011

Mbumbumbu wa Teknohama

Mbumbumbu wa teknohama, wasipewe uongozi,
Hao sawa na vilema, kujihimu kwao kazi,
Wanaongeza gharama, za maisha pia kazi,
Mbumbumbu wa Teknohama, wasipewe uongozi!!

Ya jana hawakusoma, wayashangaa ya juzi,
Wameghairi ulama, na hawajiendelezi,
Wazidi kubaki nyuma, dunia ya utandawazi,
Mbumbumbu wa Teknohama, wasipewe uongozi!!

Ni wafanyabiashara, wameshika maongozi,
Mkongo umetuama, sababu ya shinikizi,
Wanasiasa daima, nyuma kama madoezi,
Mbumbumbu wa Teknohama, wasipewe uongozi!!

Hawa wetu maamuma, hawaijui ngamizi,
Kompyuta walalama, imewashinda ujuzi,
Ustawi na salama, mashakani tumaizi,
Mbumbumbu wa Teknohama, wasipewe uongozi!!

Kiongozi kumtema, kama aleta ajizi,
Kuidaka na kusoma, teknohama kwa mapenzi,
Na kisha kuisukuma, tufanze mapandikizi,
Mbumbumbu wa Teknohama, wasipewe uongozi!!

Serikali imekwama, mikoani ni uchizi,
Wavuti zimesimama, kisa pesa na malezi,
NI mengi yamesamama, maendeleo na kazi,
Mbumbumbu wa Teknohama, wasipewe uongozi!!

Ingepaa teknohama, sisi si Rwanda wazuzi,
Mashariki ingetetema, kwa vyuo na maandalizi,
Wanafunzi wangehama, mamia wakapata kazi,
Mbumbumbu wa Teknohama, wasipewe uongozi!!

Bungeni kuna tuhuma, ni wapinzani wajuzi,
Kulala wanawasakama, hao kinamapinduzi,
Huropoka si kusema, na tafiti si wajuzi,
Mbumbumbu wa Teknohama, wasipewe uongozi!!

Wengine ni kinamama, vyeo kwao fumanizi,
Kwa za uongo tuhuma, leo wamepewa kazi,
Hivi ndivyo tulivyo nyuma, kujivua hatuwezi,
Mbumbumbu wa Teknohama, wasipewe uongozi!!

Sitini ikisimama, ni vigumu ugunduzi,
Ila walo na karama, awapendao Mwenyezi,
Arobaini ya heshima, kuwa wetu kiongozi,
Mbumbumbu wa Teknohama, wasipewe uongozi!!

Kwa busara na hekima, arobaini yakidhi,
Asizidi kuegema, bado awe mvumbuzi,
Abuni yenye neema, yatokee mageuzi,
Mbumbumbu wa Teknohama, wasipewe uongozi!!

No comments: