Wednesday, October 19, 2011

Elimu bila kisomo

Kasomeshwa Uingereza, mtoto wa Mfalme,
Swaziland naiwaza, si Switzerland dume,
Miaka kaipoteza, ilisha kama umeme,
Elimu kwa Mfalme, haikubadili kitu!


Kafaulu Kiingereza, na kujifanya mtume,
Kadhalika ameweza, kuwa wa wake wengi mume,
Uchumi kauupuza, nchi yafa kwa ukame,
Elimu kwa Mfalme, haikubadili kitu!

Selemani atamweza, ni kwa vipi ajitume,
Nabii aliyaweza, kwa kuupata utume,
Mwenyezi alichoagiza, hakwenda nacho kinyume,
Elimu kwa Mfalme, haikubadili kitu!

Shaka alishaongoza, akafanya ya kiume,
Dola aliisambaza, ufalme usimame,
Uzulu hakuidumaza, acha vibaraka waseme,
Elimu kwa Mfalme, haikubadili kitu!

Ukimwi unaunguza, kulia hadi kuume,
Nchi inakuwa giza, mpaka wa nje waseme,
Afrika inaiza, vipofu wetu madume,
Elimu kwa Mfalme, haikubadili kitu!

Uongozi ninawaza, tuwatume watutume?
Na mambo wanayofanza,hata wangekuwa watume,
Kuwavumilia twakwazwa,au huu mfumo dume?
Elimu kwa Mfalme, haikubadili kitu!

Kuongoza si kucheza, wanawake, wanaume,
Nchi kuiendeleza, hili kwalo msikwame,
Nafasi mkipotza, ni budi nasi tugome,
Elimu kwa Mfalme, haikubadili kitu!

Hatuwapi kuongoza, ili nyie mjinome,
Sisi mnatupuuza, ni lazima tulalame,
Hasira zikipaaza, mtakuwa pakashume,
Elimu kwa Mfalme, haikubadili kitu!

Tanzania naapiza, tabia mbaya msome,
Watu wao wanaokwaza, urafiki nao mkome,
Wanaizaya kuiza, nchi zisiwe mahame,
Elimu kwa Mfalme, haikubadili kitu!

Ni lazima kuongoza, kwa mifano ya mitume,
Wabaya kupatiliza, Mola kazi atutume,
Wazungu kujigeuza, haifai tuwateme,
Elimu kwa Mfalme, haikubadili kitu!

Na desturi za giza, ni lazima tuzichome,
Kila mtu anaweza, kuzaa jike na dume,
Balaa twazisogeza, twalaniwa na mitume,
Elimu kwa Mfalme, haikubadili kitu!

Tuondoke kwenye giza, watu pumzi waheme,
Anasa kuzipuuza, wacheni watukoromee,
Ukweli naueleza, vinginevyo msiseme,
Elimu kwa Mfalme, haikubadili kitu!

Hali inatutatiza, nchi zetu ni ukame,
Bei zinatuunguza, wanawake kwa waume,
Nyie bado mwatuteza, sasa wapi tukaseme?
Elimu kwa Mfalme, haikubadili kitu!

Mapinduzi twahimiza, wake na wanaume,
Afrika kuuguza, njaa, dhiki na ukame,
Ufukara watukwaza, viongozi si madume,
Elimu kwa Mfalme, haikubadili kitu!

Vijana tutawaponza, waje watumie sime,
Nchi zinavyozidi oza, hakuna mswalie mtume,
Haya tuache puuza, sisi sote tujitume,
Elimu kwa Mfalme, haikubadili kitu!

Tujitume kuongoza, tusiwe mapaka shume,
Maisha kuyapooza, tusigeuke magome,
Hatari kupatiliza,na amani isikome,
Elimu kwa Mfalme, haikubadili kitu!

No comments: