Saturday, October 1, 2011

Usipothamini wako, unamthamini nani?

Humthamini wa kwako, nani utamthamini?
Yawapi yako mashiko,uishe wako uduni,
Usipokipenda chako,atapenda mtu gani?
Usipothamini wako, unamthamini nani?

Maisha kama kivuko, ng'ambo hatujaiwini,
Viongozi wako huko, raia nyuma twalani,
Walao wana kicheko, wenye njaa mashakani,
Usipothamini wako, unamthamini nani?

Ninaimba sikitiko, dunia hii wageni,
Hata nje tuendako, wenyewe hatujithamini,
Na nyumbani walioko, wajiona hayawani,
Usipothamini wako, unamthamini nani?

Na wageni watokako, twadhani kuna thamani,
Hata ngumbaru waliko,twadhani watu makini,
Twaletewa mbwa koko,kwetu simba tunabuni,
Usipothamini wako, unamthamini nani?

Hamnazo walioko, tunawapa udhamini,
Twasutwa na hangaiko,sisi twajiona nyani,
Wataalamu walioko,twawaona mgagani,
Usipothamini wako, unamthamini nani?

Twavitamani viboko, kama vya Mjerumani,
Eti wezi na mchoko, wenetu mashirikani,
Wawekezaji waliko, watawapa kazi gani?
Usipothamini wako, unamthamini nani?

Na ukweli ulioko, uongozi si makini,
Kushindwa wao mfuko, si wafuasi wa chini,
Kuwajibika kituko, kwa hawa wetu watani,
Usipothamini wako, unamthamini nani?

Wajibu daima wako, kuhamishwa si yakini,
Gawa madaraka yako,wajibu haiwezekani,
Dhima msimamo wako, au anguko amini,
Usipothamini wako, unamthamini nani?

No comments: