Monday, October 31, 2011

Sawaka

Eti katumwa na mzuka, sawaka anazunguka,
Sumu yake kaitwika, kwenye jino kaiweka,
Kila anapopachika,mauti hupumzika,
Sawaka wa Afrika, sumu wameneemeka!

Sumu wameneemeka, sawaka wa Afrika,
Hasira zikiwashika, ovyo wanaitapika,
Kokote huipachika, hata kwa waliowaweka,
Sawaka wa Afrika, sumu wameneemeka!

Na wanakoathirika, ni kule wanakoleleka,
Aidha huaminika, sumu imeshawatoka,
Nyumbani ukiwaweka, salama haitatoweka,
Sawaka wa Afrika, sumu wameneemeka!

Neno husambaratika, pale wanapo kurupuka,
Wengine juu huruka, mijino kuichomeka,
Watu wakahamanika, wasiweze kutimka,
Sawaka wa Afrika, sumu wameneemeka!

Kaskazini hutoka, hadi kusini kufika,
Sio wa kuaminika, hawawezi kufugika,
Bora porini kuweka, na chatu kukutanika,
Sawaka wa Afrika, sumu wameneemeka!

Mishipa imenitoka, nyoka anavyoogopeka,
Na akifa hufufuka, akazidi kukusaka,
Vigumu kuelezeka, ni kioja cha hakika,
Sawaka wa Afrika, sumu wameneemeka!

Rahisi kuterereka, utelezi ukiweka,
Kutamba huja kuchoka, na misuli kumvuka,
Chini akajibweteka, na kichwa kikamtoka,
Sawaka wa Afrika, sumu wameneemeka!

Mauti yakimfika, pumzi hupumzika,
Kichwa akishakatika, hawezi kuja fufuka,
Na mkia ukiondoka, nduguze hawatamzika,
Sawaka wa Afrika, sumu wameneemeka!

No comments: