Thursday, October 20, 2011

Waachie njia nyeupe

KABLA hujamalizia, hujifanya wanajua,
Maamuzi kuamua, nusu yasiyofikia,
Matokeo yake huwa, kama tunavyoyajua,
Wajifanyao wajua, waachie nyeupe njia.

Fahamu si kusikia, yataka kuyaelewa,
Kuona na kuambiwa, haviwezi kuwa sawa,
Hujua unachojua, pia usichokijua,
Wajifanyao wajua, waachie nyeupe njia.

Afanzaye kwa kusikia, naye ni kama mbeya,
Husema asilojua, kama vile anajua,
Na hili wapaswa jua, binadamu kajaliwa,
Wajifanyao wajua, waachie nyeupe njia.

Mijini wanavyoingia, au wanapoajiriwa,
Vyeo wakifumania, hujisikia wajua,
Lakini hapana mjua, ila yule anayejua,
Wajifanyao wajua, waachie nyeupe njia.

Lataka kunyenyekea, hujui upate jua,
Si budi kutangazia, wengine watahadithia,
Ukimya huongea, na wengi hili wajua,
Wajifanyao wajua, waachie nyeupe njia.

Wapole wanaojua, kelele huzikataa,
Polepole huongea, taahira utadhania,
Ila huyapangilia, ujue usichokijua,
Wajifanyao wajua, waachie nyeupe njia.

Wajifanyao wajua, maneno huyadakia,
Maana hawajaelewa, waanza kuelezea,
Na katikati ya njia, hujikuta hawajajua,
Wajifanyao wajua, waachie nyeupe njia.

Wepesi wa kutangulia, wengine kusimulia,
Mji hawajaingia, ramani hukuelezea,
Nchi wanaisikia, kufika watakwambia,
Wajifanyao wajua, waachie nyeupe njia.

Mtu hawajamjua, watasema wamjua,
Na sifa kumsifia, au huja muumbua,
Uongo kumzulia, ukweli ukadhania,
Wajifanyao wajua, waachie nyeupe njia.

Waepuke watu hawa, acha nao kutembea,
Ogopa kuwasikia, dhambi utajichumia,
Na mtu mwenye staha, marafiki huchagua,
Wajifanyao wajua, waachie nyeupe njia.

No comments: