Tuesday, October 18, 2011

Chama au nchi

Chama kikundi cha watu, maslahi watafuta,
Kula yao sio yetu, kukosa kwao kupata,
Na kwao ujinga wetu, manufaa wanaita,
Kuimarika kwa chama, si kuimarika nchi.


Angalia hali yetu, hakika ni ya ukata,
Wanavyopewa wenzetu, sisi twabaki twaota,
Twakimbilia upatu, matatani twajikuta,
Kuimarika kwa chama, si kuimarika nchi.

Kama ni mtoto wetu, cheo hawezi kupata,
Wakwao akiwa butu, ni lazima atapeta,
Tumetupwa kwenye msitu, wa sahau na utata,
Kuimarika kwa chama, si kuimarika nchi.

Hujiita ni wenzetu, sio katika kupata,
Cha kwao si cha kwetu, chao hatuwezi chota,
Ila wasomba cha kwetu,kwa mikwara na matuta,
Kuimarika kwa chama, si kuimarika nchi.

Viongozi watukutu, chama wakishakipata,
Hujiaa kama kifutu, na kutisha kuwang'ata,
Serikali huwa butu, wachache watakaopata,
Kuimarika kwa chama, si kuimarika nchi.

Mizania iwe yetu, viwili kujavipata,
Faida kwa nchi yetu, iwe sote tunapata,
Kisha viongozi wetu, pande zote kutafuta,
Kuimarika kwa chama, si kuimarika nchi.

Na siasa kama kifutu, ukishika utajuta,
Hasa kama una kutu, huku bado unanata,
Kuna papa nao chatu, chakula wakikukuta,
Kuimarika kwa chama, si kuimarika nchi.

Nimekwama kwenye gutu, msaada ninatafuta,
Na wa mbili si wa tatu, kutembea si kunyata,
Na wenye akili katu, uchama kwao husita,
Kuimarika kwa chama, si kuimarika nchi.

Namsihi Muqsitu, nisije nami kudata,
Nivae vyake viatu, yenye kheri kuyapata,
Akinilinda na watu, shetani hatonipata,
Kuimarika kwa chama, si kuimarika nchi.

No comments: