Saturday, October 1, 2011

Warudi chini wa juu, wa chini waende juu!

Hili ni kubwa juzuu, wanafiki wasahau,
Dezodezo na bahau,halina kwao nafuu,
Lataka washikadau,vichwa visivyo mafuu,
Warudi chini wa juu, wa chini waende juu!

Anayajua mkuu, na wala halisahau,
Lilo chini kuja juu, apenda wasifu huu,
Na ni pekee Barruu, anayebaki wa juu,
Warudi chini wa juu, wa chini waende juu!

Na wanapojisahau, na kufanza ya dharau,
Yaa ayyuu anasuu, huwashika kwa miguu,
Kwa wepesi wa kifuu, ikawa juu miguu,
Warudi chini wa juu, wa chini waende juu!

Manowari na madau, na wadogo na wakuu,
Silka hii tambuu, nenda kawape nukuu,
Na wala si makuruhu, hii ni yake hukumu,
Warudi chini wa juu, wa chini waende juu!

Unyenyekevu si kiu, maji yake si limau,
Ujibari na makuu, kiumbe kwake juzuu,
Na upya si kuukuu, haachi kuyadharau,
Warudi chini wa juu, wa chini waende juu!

Siasa zina dharau, kujiona ziko juu,
Hujiona bei juu, kama adimu zambarau,
Huishi kwa chauchau, kabisa kujisahau,
Warudi chini wa juu, wa chini waende juu!

Yajayo huwa ghaibu,kama vile dafrau,
Iliki si kitunguu, na mkono si mguu,
Lau kama si nafuu, na majuto mjukuu,
Warudi chini wa juu, wa chini waende juu!

Wananchi njooni juu, waende chini wa juu,
Si laiki ya kifuu, nazi kudai ni dafu,
Hatuyataki malau,wa chini na waje juu,
Warudi chini wa juu, wa chini waende juu!

Na katiba ni juzuu, wananchi washika dau,
Kuiandika yajuzu,si serikali wakuu,
Kitabu kiwe msahafu,pasiwe wa kudharau,
Warudi chini wa juu, wa chini waende juu!

No comments: